
“Ninailinda nchi dhidi ya Adui wote, nashiriki kutunza amani duniani, Kwa maafa, majanga, huduma na hali mbaya natoa msaada na ushirikiano” .
Naam hayo ni maneno adhimu na ya kizalendo ambayo huimbwa kwa hisia katika ubeti wa pili kwenye wimbo wa Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania.
Ubeti huo una akisi mpango wa umoja wa Umoja Mataifa wa Idara ya Masuala ya Kisiasa na Ujenzi wa Amani (DPPA) unaolenga kuzuia, kusuluhisha na kudhibiti migogoro ya kisiasa kwa njia ya amani, ambapo kikundi hiki kutoka Tanzania Mei 29, Mwaka 2026 kiliungana na walinda amani wengine zaidi ya laki sabaa 700000 duniani kote katika mishei 11 za Umoja mataifa kuadhimisha Siku ya Walinda Amani Duniani.
Upendo na msaada mkubwa wa walinda amani
“Imeshapita miaka zaidi ya kumi. Ndugu zetu wa Tanzania walipoteza. Wanajeshi wao na askari. Nasema pole. Sababu kama mtu anatoka nchi nyingine anakuja kusaidia na anapoteza maisha. Ule ni upendo mkubwa wa hiyo nchi pamoja na kwa nchi ya kwetu.”
Hiyo ni kauli ya Chifu Jacque Manoku wa kata ya Matembo, vilipo Vikundi vya MONUSCO Mjini Mavivi, alipokuwa akizungumzia namna walinda amani kutoka Tanzania wanavyoendelea kujitoa na hata kupoteza maisha wakati wakitekeleza jukumu la ulinzi wa amani nchini humo DRC. Ameongeza kuwa
“Na hata wanatuma maaskari wao kuja kutusaidia. Zaidi sana Watanzania ambao tumekuwa nao kwa siku nyingi mpaka sasa tumefika kwa TANZBATT ya kumi na mbili. Tumefika tena kwa wale makomandoo TANZQRF-05. Ambao nao wanakuja tu kwa kutaka kutusaidia, kwa kweli nawashukuru na nimeona ukimya imekuja. “
Chief Manoku ameendelea kupongeza ushirkiano bora ambao umekuwa na tija baina ya kikundi hicho na Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao umeleta tija kubwa.
Mchango wa shughuli za maendeleo na ujasiriamali
Ukiachilia mbali doria za kiusalama zinazofanywa, Kikundi hiki cha TANZQRF-05 kimeendelea kushirikiana na wakaazi wa mji we Beni na Mavivi katika shughuli mbali mbali za kijamii kwakuwa ustawi wa maisha kwa raia hao ndio kipaumbele Kama anavyoeleza Kaimu Kamanda Kikosi cha TANZQRF 05 Meja Wenseslaus Mayoka.
“Tunashirikiana na wananchi katika mambo mbalimbali, tumeweza kuwafundisha mambo ya ujasiriamali, wameweza kusoma masomo ya kompyuta. Vile vile tumetoa elimu, matibabu na vifaa tiba katika zahanati mbalimbali za maeneo haya. Vile vile tumekuwa tukishirikiana na wananchi wa DRC katika michezo Mbalimbali tunawaalika ndani ya kambi yetu kuja kucheza michezo na vile vile na sisi wenyewe tunatoka nje kwenye vijiji vinavyozunguka. Tunacheza michezo mbalimbali hasa mpira wa miguu.”
Kauli za raia wa DRC kwa walinda amani
Maneno ya Meja Mayoka, yanachagizwa zaidi na raia wakaazi wa Beni Mavivi kwa namna ambavyo wamekuwa wakinufaika na uwepo wa walinda amani hawa Nchini humo
“Kwa majina naitwa Masca Sanane. Wale Watanzania wanaokuja hapa Congo wametusaidia sisi kina mama kuweza kujitegemea, kushona, kusuka nywele ,kupika chakula,wametuonesha sisi ina mama ambavyo tunaweza kujitegemea”
Shukran hizo sio kwa Masca pekee “Kwa majina naitwa Fredrick Kalunga, Graci Wametusaidia sana hapa mjini mwetu na Kijiji chetu, watu wengi tunakuja wametusaidia kwa elimu, kujifunza kushona, kujifunza kama kuranda mbao, wengi wamesahafahamu hiyo kazi. Wengiwetu hivi juzijuzi tumemaliza masomo ya kujua kompyuta, hiyo imetusaidia sana na sisi kama wakaazi vijana tumesha saidiwa, kwa kupata hiyo elimu mbalimbali tofauti ambayo tumepewa na hao watu.”
Walinda amani zaidi ya elfu 4,300 kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa wamepoteza maisha yao katika jukumu hilo tangu 1948 kutoka katika zaidi ya nchi 120 wakiwemo Watanzania wakati wakitekeleza jukumu hilo, la ulinzi wa amani.
