Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani WMO iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi, kuna uwezekano wa asilimia 80 kwamba hali ya El Niño itajitokeza kati ya mwezi Juni na Agosti, na uwezekano huo kuongezeka hadi asilimia 90 katika kipindi kitakachofuata.

El Niño ina athari duniani kote

“Ujumbe huu ni muhimu kwa sababu El Niño ni moja ya vichocheo vikuu vya mifumo ya hali ya hewa na tabianchi duniani,” amesema Katibu Mkuu wa WMO, Celeste Saulo katika ripoti hiyo.

Ameeleza kuwa athari za El Niño haziishii katika Bahari ya Pasifiki pekee bali huathiri kilimo, usambazaji wa nishati, biashara, rasilimali za maji, minyororo ya ugavi na maisha ya watu katika maeneo mengi duniani.

Kwa sasa, halijoto ya Bahari ya Pasifiki ya kitropiki iko juu kwa nyuzi joto 6 za celsiasi kuliko wastani wa kawaida, jambo linaloongeza wasiwasi kuwa El Niño hii inaweza kutumia joto hilo la ziada na kusababisha madhara makubwa kwa jamii zilizo hatarini na ambazo hazijajiandaa vya kutosha.

© UNICEF/Sukhum Preechapanich Watoto nchini Thailand wanastahimili joto kali sana na ukame

Joto la dunia na matukio mabaya ya tabianchi

Bi. Saulo amekumbusha kuwa El Niño ya mwaka 2023–2024 ilikuwa miongoni mwa tano zenye nguvu zaidi kuwahi kurekodiwa na ilichangia kwa kiasi kikubwa kuvunjwa kwa rekodi za joto duniani mwaka 2024.

Kwa mujibu wa WMO, hakuna ushahidi kwamba mabadiliko ya tabianchi yanaongeza mara kwa mara au nguvu ya matukio ya El Niño. Hata hivyo, mabadiliko hayo yanaweza kuongeza athari zake kwa sababu bahari na angahewa zenye joto zaidi hubeba nishati na unyevunyevu mwingi zaidi unaochochea matukio makali kama mawimbi ya joto na mvua kubwa.

Kujiandaa mapema ni muhimu

“Tunaielewa El Niño, tunaweza kujiandaa vizuri zaidi kwa El Niño kutokana na sayansi na uwekezaji uliofanywa na nchi nyingi katika maandalizi,” amesema mkuu huyo wa WMO akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva.

Ameongeza kuwa pamoja na El Niño, dunia inaendelea kushuhudia matukio mengine mabaya zaidi ya hali ya hewa ambayo yanahitaji uwekezaji mkubwa zaidi ili kupunguza madhara yake.

Katika miezi ijayo, WMO kwa kushirikiana na taasisi za hali ya hewa duniani itaendelea kufuatilia maendeleo ya hali hiyo ili kusaidia serikali, mashirika ya kibinadamu na sekta nyingine zinazotegemea taarifa za tabianchi kufanya maamuzi sahihi.

“Utabiri wa msimu unaotolewa mapema pamoja na mifumo ya tahadhari za mapema ni muhimu katika kuokoa maisha na kupunguza athari kwa uchumi wetu na jamii zetu,” amesisitiza Bi. Saulo.

El Niño na La Niña ni nini?

El Niño na La Niña ni awamu mbili zinazopingana za mfumo unaojulikana kama El Niño–Southern Oscillation (ENSO), ambao ni miongoni mwa mifumo yenye nguvu zaidi ya tabianchi inayotokea kiasili duniani.

El Niño hutokea pale ambapo joto la uso wa bahari katika sehemu za kati na mashariki mwa Bahari ya Pasifiki ya Ikweta huongezeka kuliko kawaida. 

Kwa kawaida hutokea kila baada ya miaka miwili hadi saba na hudumu kwa takriban miezi tisa hadi 12.

Mara nyingi huanza kujitokeza kati ya Machi na Juni, kufikia kiwango chake cha juu kati ya Novemba na Februari, huku athari zake kwa halijoto ya dunia zikionekana zaidi katika mwaka wa pili baada ya kuanza kwake.

Viwango vya El Niño

Matukio ya ENSO hugawanywa katika makundi manne, dhaifu, wastani, yenye nguvu na yenye nguvu sana.

WMO imeonya kuwa hata El Niño ya kiwango cha wastani inaweza kuongeza uwezekano wa kutokea kwa matukio mabaya ya hali ya hewa na tabianchi katika maeneo mbalimbali duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *