KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga amesema atatumia mapumziko ya siku 14 kuimarisha safu ya ulinzi na ushambuliaji wa timu hiyo katika harakati za kujinasua kutoka hatari ya kushuka daraja.
Mbeya City inaendelea na mazoezi licha ya kusimama kwa Ligi Kuu kutokana na kalenda ya FIFA ikiwa haipo kwenye sehemu nzuri katika msimamo wa ligi.
Timu hiyo ipo nafasi ya 14 na pointi 22 na imefungwa mabao 39 ikiwa timu ya pili kuruhusu mabao mengi kwenye ligi hadi sasa nyuma ya KMC.
Mayanga amesema changamoto kubwa aliyoikuta ni timu kuruhusu mabao mengi, jambo analolifanyia kazi sambamba na kuongeza makali ya ushambuliaji.
“Nimeamua kuvunja mapumziko ili kurekebisha makosa. Tunaruhusu mabao mengi na hilo ndilo eneo kubwa tunalofanyia kazi kwa sasa,” amesema Mayanga.
“Ninaamini katika mechi tano zilizobaki tutakuwa timu tofauti bado tunaweza kufanya vizuri msimu huu.”
Mwishoni mwa msimu wa ligi timu mbili zinashuka moja kwa moja, huku mbili zikicheza michezo ya mtoano zenyewe kwa zenyewe, itakayoshinda itacheza mechi mbili za mtoano na timu kutoka Championship kupata timu moja itakayokwea Ligi Kuu Bara.