Dar es Salaam. Wasanii wa muziki Tanzania, wameelezea kushtushwa na kifo cha msanii mkongwe wa Hip Hop na Bongo Flava, Zaynab Lipangile maarufu kama Zay B, aliyefariki dunia Mei 31, 2026 akiwa nyumbani kwake Temeke jijini Dar es Salaam na kuzikwa siku hiyohiyo katika makaburi ya Tabata Kinyerezi.

Kwa mujibu wa familia yake, Zay B alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa vidonda vya tumbo kwa muda mrefu, ugonjwa unaotajwa kuchangia kifo chake. 

Msanii mkongwe wa Hip Hop, Juma Nature, amesema kifo hicho hakukitegemea kutokana na historia ndefu aliyokuwa nayo na marehemu kwenye muziki.

“Ni habari ya kusikitisha sana kwa sababu alikuwa mmoja wa wasanii waliopambana kuujenga muziki wetu katika kipindi ambacho kila kitu kilikuwa kigumu. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi,” amesema Juma Nature.

Soggy Dog amesema kuwa atakumbuka jitihada za Zay B katika muziki.

“Dada yetu ametuacha mapema, apumzike kwa amani Zainab. Nakumbuka ulikuwa dada shuleni pale Meta, na kwa kweli najivunia kuona nilivyokuchochea na kukuvuta kwenye muziki hadi ukatengeneza historia yako mwenyewe kwenye Bongo Fleva,” amesema Soggy.

Kwa upande wake, Squeezer alisema, “Zay B kwangu hakuwa rafiki wa kawaida, alikuwa kama ndugu yangu wa karibu sana. Tulikuwa tunaishi jirani eneo la Kinyerezi, hivyo tulikuwa karibu muda mwingi. 

“Alikuwa msichana mwenye moyo wa kupambana, ingawa kwa muda mrefu alisumbuliwa sana na ugonjwa wa vidonda vya tumbo.”

Suma G alisema atamkumbuka Zay B kwa mchango wake kwa muziki wa kizazi kipya.

“Zay alikuwa rafiki mzuri sana na miongoni mwa wasanii wa kike wakongwe walioweza kuitikisa Bongo Fleva. Alikuwa mpambanaji wa kweli, mtu ambaye hakupenda kushindwa katika game. Historia yake kwenye muziki itaendelea kumkumbusha kama mmoja wa wanawake walioweka msingi wa muziki wetu,” amesema Suma G.

Zay B anakumbukwa zaidi kupitia nyimbo zake zilizotikisa mwanzoni mwa miaka ya 2000 ikiwamo ‘Nipo Gado’ aliyomshirikisha Inspector Haroun, wimbo ambao baadaye ulipata umaarufu zaidi kupitia remix iliyomhusisha Juma Nature. Pia aliwahi kufanya vizuri kupitia nyimbo kama ‘Monica’, ‘Ananitesa’ aliyowashirikisha Unique Dadaz na Odinali pamoja na Banana Zoro.

Mbali na nyimbo hizo, Zay B aliwahi kuachia albamu ya ‘Mama Africa’ iliyofanya vizuri katika soko la muziki wakati huo na kumfanya kuwa miongoni mwa wasanii wa kike waliokuwa wakitikisa katika kizazi cha kwanza cha Bongo Fleva.

Katika safari yake ya muziki, Zay B alijizolea umaarufu mkubwa kutokana na uwezo wake wa kurap na ushindani wake wa kisanaa na rapa mwenzake Sister P, jambo lililokuwa gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki wa muziki wa kizazi kipya nchini na kuchochea maendeleo ya Hip Hop ya Tanzania.

Ingawa katika miaka ya baadaye alipunguza shughuli zake za muziki na kuonekana mara chache hadharani, Zay B ataendelea kukumbukwa kama mmoja wa wanawake walioweka msingi imara wa muziki wa Bongo Fleva na Hip Hop nchini, huku mchango wake ukiendelea kuishi kupitia kazi alizoziacha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *