ARUSHA: SERIKALI imesema kuwa zaidi ya asilimia 70 ya fedha zinazohitajika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 zinatarajiwa kutoka sekta binafsi, huku Mfuko wa Kukuza Ukuaji wa Uwekezaji Tanzania (TIGF) ukizinduliwa kama jukwaa la kuandaa miradi na kuunganisha fursa za maendeleo na mitaji ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, wakati akifungua Kongamano la Uwekezaji Tanzania 2026 kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, jijini Arusha.

Kairuki amesema TIGF ni jukwaa kuu la kitaifa la kuandaa miradi na kurahisisha uwekezaji, likiwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha mitaji kwa ajili ya vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania.

Tanzania ipo katika nafasi nzuri ya kuvutia uwekezaji mkubwa utakaosaidia kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku akisisitiza umuhimu wa sekta binafsi katika kugharamia miradi ya maendeleo.

Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Mipango na Uwekezaji, Dk. Pius Chaya, amesema kongamano hilo ni sehemu ya juhudi za serikali za kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo kupitia ushiriki mkubwa wa sekta binafsi.

Ameongeza kuwa serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuimarisha uratibu wa taasisi, kuboresha mifumo ya kisheria na kuweka mazingira yanayowawezesha wawekezaji kufanya maamuzi kwa uhakika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii(ESRF) Profesa, Fortunata Makene, amesema kuanzishwa kwa TIGF ni hatua muhimu katika kushughulikia changamoto ya ukosefu wa miradi iliyoandaliwa kwa viwango vinavyokubalika na wawekezaji na taasisi za kifedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *