Arusha. Serikali imeweka mezani miradi 60 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 6.35 (Sh16.7 trilioni) kwa lengo la kuvutia mitaji ya sekta binafsi na kuharakisha utekelezaji wa malengo ya uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

Miradi hiyo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar imewasilishwa kwa wawekezaji wa ndani na nje kupitia Mkutano wa Kwanza wa Uwekezaji Tanzania 2026, unaoendelea jijini Arusha kuanzia Juni 1 hadi 2, 2026.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki amesema Serikali imeamua kuifanya sekta binafsi kuwa mhimili mkuu wa maendeleo kwa kuongeza ushiriki wake katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.

Amesema Serikali inalenga zaidi ya asilimia 70 ya fedha zinazohitajika kutekeleza vipaumbele vya maendeleo kutoka kwa wawekezaji binafsi ili kupunguza utegemezi wa vyanzo vya kawaida vya fedha za maendeleo.

“Ili kufikia lengo la uchumi wa dola trilioni moja, tunaelekeza nguvu katika mifumo bunifu ya ufadhili ikiwemo ufadhili mseto, ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) pamoja na ushiriki mkubwa wa sekta binafsi katika miradi ya maendeleo,” amesema Kairuki.

Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka wazi kuwa ufadhili mbadala si chaguo tena bali ni hitaji muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya nchi.

Kwa mujibu wa Kairuki, thamani ya miradi iliyowasilishwa imeongezeka kutoka dola bilioni 2.85 (Sh7 trilioni) zilizokuwa zimeandaliwa awali hadi kufikia dola bilioni 6.35 (Sh16.7 trilioni), jambo alilosema linaonyesha kuongezeka kwa imani ya wawekezaji pamoja na mafanikio ya Serikali katika kuandaa miradi yenye mvuto wa kifedha.

“Hatuko hapa kwa ajili ya mazungumzo pekee, tuko hapa kufanya maamuzi yatakayobadilisha miradi kuwa uwekezaji halisi na mikataba ya kifedha,” amesema.

Miradi hiyo inahusisha sekta za uchumi wa buluu, maji na usafi wa mazingira, usafirishaji na logistiki, utalii, miundombinu ya asili pamoja na teknolojia ya habari na mawasiliano.

Kairuki amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara kupitia majukwaa kama Tanzania Investment Growth Facility (TIGF), yanayolenga kuhamasisha mtaji, kujenga ushirikiano wa kimkakati na kuharakisha utekelezaji wa uwekezaji katika sekta muhimu za uchumi.

Mkutano huo umeandaliwa na Tanzania Investment Growth Facility (TIGF) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP Tanzania).

Washiriki wa mkutano huo ni pamoja na taasisi za fedha za maendeleo, benki za biashara, mifuko ya pensheni na wawekezaji binafsi kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dk Steven Shayo amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kujenga uchumi wenye ushindani mkubwa unaotegemea uzalishaji, uongezaji thamani, ubunifu na ushiriki mpana wa sekta binafsi.

Amesema Serikali inaendelea kuimarisha sera, uratibu wa taasisi na mazingira ya biashara ili kuhakikisha miradi inayotokana na majadiliano ya uwekezaji inatekelezwa na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Shigeki Komatsubara amesema dunia inaelekea katika mfumo mpya wa maendeleo unaozingatia uwekezaji endelevu badala ya kutegemea misaada ya kifedha.

Amesema changamoto kubwa kwa nchi nyingi si ukosefu wa fedha duniani bali ni uhaba wa miradi iliyoandaliwa vizuri na inayoweza kuvutia wawekezaji.

“Afrika ina rasilimali nyingi, vipaji na fursa. Changamoto kubwa ni kuwa na miradi inayokidhi mahitaji ya wawekezaji na taasisi za fedha,” amesema.

Ameipongeza Tanzania kwa kuandaa miradi inayoweza kufadhiliwa na kuunganishwa moja kwa moja na wawekezaji badala ya kuendelea kutegemea misaada ya nje.

Naye Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji wa Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi Tanzania (TISEZA), George Mukono amesema Serikali inaendelea kuandaa maeneo ya viwanda yenye miundombinu tayari kwa ajili ya wawekezaji huku changamoto ya upatikanaji wa ardhi ikiendelea kuhitaji ufumbuzi wa haraka.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Profesa Fortunata Makene amesema mafanikio ya uwekezaji endelevu yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na binafsi.

Amesema mkutano huo umeundwa kuimarisha orodha ya miradi ya uwekezaji ya Tanzania na kugeuza maono ya maendeleo kuwa matokeo halisi ya kiuchumi kupitia ushirikiano wa kimkakati na vyanzo vipya vya ufadhili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *