
Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, na baadhi ya wadau na mashabiki wa soka nchini, wamewasili salama jijini Casablanca, Morocco asubuhi hii, Juni 2, 2026.
Taifa Stars ipo Morocco kwa ajili ya mechi mbili za kirafiki za kimataifa zilizopangwa kupigwa wiki hii.
Kikosi cha Stars kitaelekea mjini Marrakech ambapo kitashuka uwanjani kupimana nguvu dhidi ya timu za Uganda na Rwanda, michezo inayolenga kuimarisha kikosi hicho kwa mashindano yajayo.
Hata hivyo, mashabiki wote walioambatana na msafara huo wataenda jijini Rabat kwa kazi maalum ya kuipa nguvu timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’.
Serengeti Boys inashuka dimbani usiku wa leo Jumanne, Juni 02, 2026, kuwania ubingwa wa Afrika.
Serengeti Boys itachuana na timu ya vijana ya Senegal katika mchezo wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17).
Mtanange huo wa kukata na shoka unatarajiwa kuanza saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Serengeti Boys imeingia hatua ya fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 4-3 dhidi ya Misri kwenye nusu fainali.
Senegal imetinga hatua ya fainali baada ya kushinda kwa mikwaju ya penalti 7-6 dhidi ya Morocco katika mchezo mwingine wa nusu fainali.