
WHO, nchini Lebanon inafanyia uthibitisho taarifa za mashambulizi yaliyolenga hospitali katika mji wa Tyre jana Jumatatu, huku kukiwa na ongezeko la kutia wasiwasi la mashambulizi dhidi ya vituo vya afya nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka mamlaka za Lebanon, watu wasiopungua 86, wakiwemo wahudumu wa afya, wamejeruhiwa katika mashambulizi dhidi ya Hospitali ya Jabal Amel.
Mwakilishi wa WHO nchini Lebanon, Abdinasir Abubakar, amesema mashambulizi hayo yalisababisha uharibifu mkubwa katika idara ya dharura na chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Akizungumza kutoka mji mkuu wa Beirut leo Jumanne, Dkt. Abubakar amesema Hospitali ya Jabal Amel ni miongoni mwa hospitali chache ambazo bado zinaendelea kutoa huduma kusini mwa Lebanon.
Mashambulizi ya afya yaongezeka
Katika kipindi cha miezi mitatu pekee, WHO imethibitisha karibu mashambulizi 190 dhidi ya sekta ya afya, yaliyosababisha vifo vya wahudumu wa afya 128 na kujeruhi wengine 332. Wiki moja iliyopita pekee ilishuhudia mashambulizi 11 dhidi ya huduma za afya.
Dkt. Abubakar ameongeza kuwa “Mashambulizi haya hayasababishi tu vifo na majeraha, bali pia yanawanyima watu huduma muhimu za afya wanazozihitaji.”
Eneo la Tyre limeathirika zaidi katika siku za karibuni kutokana na mapigano kati ya wapiganaji wa Hezbollah na Israel.
Hospitali mbili kati ya tatu zilizopo katika eneo hilo, Jabal Amel na Hiram, zimeharibiwa, huku hospitali ya tatu ikilemewa na ongezeko kubwa la wagonjwa waliojeruhiwa.
Huduma muhimu za afya zatikiswa
WHO imesema upatikanaji wa huduma muhimu za afya umeathirika vibaya, hasa kusini mwa Lebanon, ambapo wagonjwa wanalazimika kusubiri hadi saa 48 kufikishwa katika hospitali za rufaa.
“Hospitali sita bado hazijaanza tena huduma za uzazi na kwa sasa zinatoa huduma za dharura pekee,” amesema Dkt. Abubakar. “Kwa wanawake wajawazito na watoto wachanga, kuchelewa kupata huduma kunaweza kuwa tofauti kati ya maisha na kifo.”
Wasiwasi wa magonjwa katika makazi ya wakimbizi
WHO pia imeelezea hali ngumu ya kiafya katika makazi ya muda yanayohifadhi takribani watu 130,000 waliokimbia mapigano.
Idadi ya waliokimbia makazi yao inaendelea kuongezeka kufuatia maagizo mapya ya watu kuhama yaliyotolewa na Israel.
Kuongezeka kwa ghasia pamoja na onyo la mashambulizi ya Israel katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, vinavyoishi mamia ya maelfu ya raia, kumesababisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili hali hiyo siku ya Jumatatu.
WHO imekuwa ikifuatilia magonjwa ya kuambukiza katika makazi ya wakimbizi na jamii zinazowahifadhi, na imebaini ongezeko la visa vya kuhara vinavyosababishwa na maji machafu.
“Tupo katika msimu wa joto na sasa hatari ya mlipuko wa kipindupindu inaweza kuongezeka,” ameonya Dkt. Abubakar.
Wito wa kulinda huduma za afya
WHO imesisitiza kuwa mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka kwa kasi kuliko uwezo wa kuyashughulikia, na hivyo kuhitajika ufadhili endelevu kwa huduma muhimu za afya.
“Tunahitaji pia mashambulizi dhidi ya huduma za afya yakome na vituo vya afya vilindwe kikamilifu,” amesema Dkt. Abubakar, akirudia wito wa kusitishwa kwa mapigano na kupatikana kwa amani ya kudumu.
Tangu kuanza kwa awamu ya sasa ya mapigano kati ya Israel na wapiganaji wa Hezbollah tarehe 2 Machi, zaidi ya watu 3,400 wameuawa nchini Lebanon na karibu watu 10,400 wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa raia.
Dkt. Abubakar amesema “Hii imekuwa baadhi ya miezi yenye vifo vingi zaidi nchini Lebanon tangu kuanza kwa mzozo mwezi Oktoba 2023,”.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyopatanishwa na Marekani kati ya Lebanon na Israel yalianza kutekelezwa tarehe 17 Aprili, lakini hayajawahi kuheshimiwa kikamilifu na pande zote mbili.
Makubaliano hayo yameongezwa mara mbili, mara ya mwisho ikiwa tarehe 16 Mei kwa kipindi cha siku 45.