Shinyanga. Wadau wa sekta ya maji mkoani Shinyanga wamepitisha na kuidhinisha mapendekezo ya marekebisho ya bei za huduma za maji safi na usafi wa mazingira yaliyowasilishwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (Shuwasa), huku Serikali ikisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi.

Akizungumza leo Jumatano, Juni 03, 2026 katika kikao cha wadau kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Kaimu Mkurugenzi wa huduma kwa wateja wa Shuwasa, Reuben Mwandumbya amesema hatua hiyo inalenga kuiwezesha mamlaka kuendelea kutoa huduma bora, salama na endelevu kwa wananchi huku ikikabiliana na changamoto za ongezeko la gharama za uendeshaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira.

Kaimu Mkurugenzi wa huduma kwa wateja wa SHUWASA, Reuben Mwandumbya akizungumza na wadau katika kikao kilichofanyika Manispaa ya Shinyanga.

“Kwa mujibu wa viwango vipya vitakavyoanza kutumika katika mwaka wa fedha 2026/2027, wateja wa majumbani wanaotumia zaidi ya mita za ujazo tano kwa mwezi watalipa Sh1,840 kutoka Sh1,740 za sasa, huku taasisi mbalimbali zitalipa Sh3,060 kwa mita ya ujazo kutoka Sh2,760 huku wateja wa sekta ya biashara wakilipa kutoka Sh2,790 hadi Sh3,100 kwa mita ya ujazo” amesema Mwandumbya.

Amesema gharama za huduma ya maji kwa viwanda zimeongezeka kutoka Sh2,850 hadi kufikia Sh3,160 kwa mita ya ujazo, wakati viwanda vya vinywaji vitatozwa Sh4,160 kutoka Sh3,750 za awali na vibanda vya kuuza maji, kiwango kipya kitakuwa Sh1,670 kwa mita ya ujazo kutoka Sh1,500 za awali.

Mwandumbya amesema marekebisho hayo yatasaidia kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama, kuboresha miundombinu ya uzalishaji na usambazaji wa maji, kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wateja pamoja na kuwezesha utekelezaji wa miradi mipya ya upanuzi wa huduma katika maeneo mbalimbali yanayohudumiwa na Shuwasa.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Shuwasa, Reuben Kitinya amesema sababu ya mabadiliko hayo ni pamoja na kupanda kwa gharama za vifaa vya uendeshaji,

Mkurugenzi mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola akizungumza na wadau ukumbi wa mkoani, uliopo Manispaa ya Shinyanga.

“Gharama hizi zimetokana na kupanda kwa mabomba, viungio, dawa za kutibu maji, vifaa vya uendeshaji na matengenezo ya miundombinu ya maji pamoja na mahitaji yanayoongezeka ya wananchi ya kupata huduma bora” amesema Kitinya.

Amesema maji safi ni hitaji la msingi kwa maisha ya binadamu, afya ya jamii, maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa mazingira, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha miundombinu ya maji inalindwa, inaboreshwa na kupanuliwa ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na huduma hiyo muhimu.

Naye, Mkurugenzi mtendaji wa Shuwasa, Mhandisi Yusuph Katopola amebainisha kuwa mamlaka hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma za maji katika Manispaa ya Shinyanga pamoja na maeneo ya Tinde, Didia na Iselamagazi sambamba na kuboresha mifumo ya utoaji huduma.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza katika kikao na wadau wa Shuwasa, kilichofanyika katika ukumbi wa mkoani, uliopo Manispaa ya Shinyanga.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ameipongeza Shuwasa kwa juhudi zake za kuendelea kuboresha huduma za maji na kusisitiza kuwa elimu kwa wananchi inapaswa kuendelea kutolewa ili waelewe sababu za mabadiliko ya bei hizo.

“Serikali imeendelea kuwekeza fedha katika miradi ya maji nchini kwa lengo la kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi wengi zaidi mijini na vijijini, pia itaendelea kusogeza huduma za maji karibu na wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati,” amesema Mtatiro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *