
Tulipokuwa watoto tulikuwa na mazoea ya kutamani vitu tofauti. Tulipowaona wenzetu wakiringa na baiskeli zao, na sisi tuliwalilia wazazi tukitaka baiskeli kama hizo. Wazazi walituahidi, lakini kutokana na mipango na matumizi yao hawakuliweka hilo kuwa kipaumbele.
Sisi hatukuchoka, tulisumbuana nao kwa kilio kilekile hadi baiskeli ikawekwa kwenye mpango wa manunuzi. Ikanunuliwa na ugomvi ukaisha.
No, ugomvi haukwisha ila hali ilitulia. Siku moja tulikuwa uwanjani tukicheza ‘chandimu’. Tukasikia mrindimo angani mithili ya dhoruba. Tahamaki bonge la dege lilionekana chini chini, likielekea kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere.
Baadaye tukaambiwa kuwa hilo lilikuwa dege la Papa. Sisi tulimwona Papa akiwa mwenye bahati kubwa kumiliki dege kama lile. Ugomvi mpya ukazaliwa: kila mmoja aliwalilia wazazi wake wamnunulie dege kama la Papa!
Pamoja na ukubwa wa ugomvi huo, hakuna hata mmoja wetu aliyefanikiwa. Tulijikatia tamaa, lakini tuliendelea kuomba siku moja wazazi watoe ahadi ya kutununulia dege hilo.
Au nalo liwe kwenye manunuzi ya kawaida kama viatu vya shule, nguo za sikukuu na kadhalika. Lakini mpaka sasa nasi tumeshakuwa wazazi, tunajua dira ya maisha inavyoshabihiana na dira ya meli.
Katika wakati huu, Watanzania wanaitazama Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa macho tofauti. Wapo wenye imani wanaosubiri matokeo, lakini pia kuna ambao hawategemei mvua bila kuona mawingu kwanza.
Hawa wanaona ndoto ya kufikia malengo ya dira, bado imezongwa na matatizo yaliyoshindikana kutatuliwa. Wanaamini itawezekana tu iwapo vikwazo vitaanza kung’olewa.
Wanaona picha ya mtoto anayelilia ndege inayosafiri angani, wakati mtoto huyo amenaswa kwenye dimbwi la tope. Ndiyo wanavyomwona mwananchi anayeahidiwa maendeleo akiwa kanasa kwenye dimbwi la umasikini.
Nadhani mtu yeyote angeulizwa juu ya nini kifanyike, angejibu kuwa la kwanza ni kumnasua mwananchi huyu. Maendeleo yasingekuwa na maana kwake kuyaona bila kuyashiriki.
Maendeleo yanapaswa kwenda sanjari na maisha ya mtu mmoja mmoja. Dira yetu inaelekeza kufikia uchumi wa kipato cha juu, ambapo pato la kila mtu linatarajiwa kufikia takribani dola 7,000 kwa mwaka.
Kiasi hicho kwa sasa ni sawa na takribani Shilingi za Kitanzania zaidi ya milioni moja na nusu kila mwezi. Kwa kiwango hiki hakuna anayebisha kuwa kukilinganisha na kipato cha Mtanzania kawaida, kila mmoja ataimba kiitikio cha “umasikini bai-bai”.
Sasa kwa kuwa dira ni chombo cha kuonesha uelekeo, meli haiwezi kuitegemea dira pekee ili kufika bandarini. Ni wajibu wa nahodha na mabaharia wake kupambana ili kukifikisha chombo salama.
Inategemewa bahari iwe shwari na chombo kiwe kwenye hali nzuri. Iwapo kuna tufani tusitegemee kuvuka. Au kama chombo kimenasa kwenye “fungu”, kamwe hatutaweza hata kwa jitihada zipi.
Ni kawaida kusafisha njia ili ipitike. Vikwazo huweza kuifanya safari iwe ngumu au isiwezekane kabisa. Ni lazima lizibwe ili mambo yaende kama yanavyotarajiwa. Vinginevyo matokeo yanaweza kuwa mabaya kiasi cha kupoteza maisha ya watu na mali.
Mtanzania wa kawaida anahangaika na vitu vya lazima maishani. Anapambana kumudu gharama za chakula, mavazi, malazi, elimu na vitu vingine vya lazima maishani.
Kwa namna fulani, anadhani kuna uwezekano akapunguziwa gharama hizi angalau atoke kwenye dimbwi la umasikini. Ni matumaini yake kuwa akijikwamua humo, hataambukiza virusi vya majanga kwa wale wanaomtegemea.
Tuseme ukweli bila kupepesa macho; Serikali imekuwa ikisambaza huduma kwa wananchi hadi kule vijijini. Shule na hospitali ambazo zilikuwa adimu nchini, sasa zipo kila mahala. Tatizo ni upatikanaji wa huduma zake kwa watu masikini. Mwamko mkubwa umeonekana kwa wazazi ambao hawakujaaliwa kupata elimu.
Wao baada ya kupitia hali ngumu ya maisha, wamekuwa na jitihada za kusomesha watoto wao ili yasiwakute yaliyomkuta.
Lakini pamoja na kutangaziwa elimu ya bure, bado anakutana na gharama zinazoweza kuzidi zile za elimu ya kulipia. Inampasa kuwalipia nauli, chakula, ulinzi, ada za mitihani na masomo ya ziada, na kadhalika.
Vivyo hivyo kwa wazazi walioelimika juu ya uzazi salama, wanakwenda kukutana na ada zisizokuwa wazi kwenye mahudhurio ya kliniki na wakati wa kujifungua. Wapo waliopoteza maisha kwa kukosa beseni wakati wa uzazi.
Hospitali haiwezi kuwa hospitali bila ya dawa. Iwapo mgonjwa analazimika kulipia matibabu kwenye hospitali ya Serikali, basi kuna tofauti gani kati ya hospitali hiyo na ile ya kulipia?
Hivi kuna uzito gani wa kuyafanya mabeseni yawe sehemu ya vifaa muhimu kwenye hospitali ya wazazi? Kwa hali hii, ipo hatari ya mgonjwa atakayeandikiwa kulazwa wodini kulazimika kwenda na kitanda chake.
Mambo haya yanaonekana kuwa madogo, lakini yanaweza kuwa mwiba wa Dira ya Taifa. Kuyaachia yaendelee ni kuyahalalisha yawe magugu kwenye mazao yetu.
Tutafika kwenye pato la dola 7,000 kwa mwaka, wakati gharama za elimu na matibabu zikizidi pato hilo. Maendeleo ya Taifa yapimwe kwa maisha ya mtu mmoja mmoja kupitia hali yake ya maisha.