Ikiwa zimebaki siku nane kuanza kwa Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika kwa pamoja katika Mataifa ya Marekani, Canada na Mexico, zipo rekodi ambazo ziliwekwa na magwiji wa soka waliopita na hadi sasa rekodi hizo bado hazijavunjwa wala kufikiwa.
Mshambuliaji wa zamani wa Brazil, Edson Arantes do Nascimento, maarufu Pelé, alipokuwa amebebwa na wachezaji wenzake katika moja ya Fainali za Kombe la Dunia. Picha na Mtandao
Rekodi ya mataji
Rekodi hii inashikiliwa na aliyekuwa mshambuliaji wa zamani wa Brazil, Edson Arantes do Nascimento, maarufu Pelé, ambaye aliacha historia ya kushinda mataji matatu ya Kombe la Dunia akiwa na Brazil.
Mshambuliaji huyo alifanikiwa kutwaa mataji ya mwaka 1958, 1962 na 1970. Mbali na kuweka rekodi hiyo, Pelé pia anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutwaa Kombe la Dunia baada ya kuiongoza Brazil kushinda taji la mwaka 1958 alipokuwa na miaka 17 na siku 249 pekee.
Mshambuliaji wa zamani wa Brazil, Edson Arantes do Nascimento, maarufu Pelé, (watatu kulia) alipokuwa na wachezaji wenzake katika Fainali za Kombe la Dunia la 1958 Sweden akiwa na miaka 17.
Pelé alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82 wakati alipokuwa akipatiwa matibabu ya kansa katika Hospitali ya Albert Einstein iliyopo Sao Paulo, Brazil.
Mbali na Pelé, yupo kipa wa zamani wa Italia, Dino Zoff ambaye ana historia ya kushinda Kombe la Dunia akiwa na umri mkubwa zaidi.
Zoff aliisaidia Italia ‘Gli Azzurri’ kutwaa ubingwa wa mwaka 1982 alipokuwa na umri wa miaka 40 siku 133 rekodi ambayo hadi sasa hakuna mchezaji aliyewahi kuifikia.
Aliyekuwa beki wa kulia wa Brazil, Marcos Evangelista de Morais, maarufu Cafu. Picha na Mtandao
Rekodi ya fainali
Aliyekuwa beki wa kulia wa Brazil, Marcos Evangelista de Morais, maarufu Cafu, anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji pekee kuwahi kucheza Fainali tatu mfululizo za Kombe la Dunia.
Beki huyo kisiki alifanya hivyo baada ya kuisaidia Brazil kutinga fainali za mwaka 1994, 1998 na 2002. Katika fainali hizo, Caf aliiongoza Brazil kushinda mataji mawili ya mwaka 1994 na 2002.
Nahodha huyo wa zamani wa Brazil alistaafu kucheza soka 2008 akiwa na umri wa miaka 38.
Mshambuliaji wa zamani wa Uturuki, Hakan Şükür. Picha na Mtandao
Bao la mapema
Mshambuliaji wa zamani wa Uturuki, Hakan Şükür yeye anashikilia rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi katika Fainali za Kombe la Dunia baada ya kutumia sekunde ya 11.
Nyota huyo alifanya hivyo katika ushindi wa 3-2 iliopata Uturuki katika mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu katika fainali za 2002 akiisaidia timu yake kuichapa Korea Kusini ambayo ilikuwa muandaaji wa michuano hiyo ikishirikiana na Japan.
Aliyekuwa mshambuliaji wa Ujerumani, Miroslav Klose. Picha na Mtandao
Aliyekuwa mshambuliaji wa Ujerumani, Miroslav Klose ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Kombe la Dunia akiwa na mabao 16 aliyofunga katika Fainali nne tofauti za Kombe la Dunia kuanzia 2002 hadi 2014.
Nyota huyo alifunga mabao matano katika fainali zilizofanyika Korea Kusini na Japan 2002, akafunga tena mabao matano katika fainali za 2006 zilizofanyika Ujerumani, kisha akafunga mabao manne kwenye fainali za 2010 Afrika Kusini kabla ya kuhitimisha kwa mabao mawili katika fainali za 2014 zilizofanyika Brazil.
Mbali na mshambuliaji huyo anayeongoza kwa mabao mengi, yupo Mfaransa Just Fontaine ambaye aliweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi katika shindano moja la mwaka 1958.
Mshambuliaji wa Ufaransa, Just Fontaine ambaye aliweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi katika shindano moja la mwaka 1958.
Katika fainali hizo zilizofanyika Sweden, Fountaine aliweka rekodi hiyo baada ya kufunga mabao 13 katika mechi sita pekee. Mshambuliaji huyo alizaliwa Agosti 18, 1933 huko Marrakesh, Morocco na alifariki Dunia, Februari 28, 2023 akiwa na miaka 89 alipokuwa Toulouse, Ufaransa.
Orodha ya Wafungaji Bora Kombe la Dunia
1. Miroslav Klose 16
2. Ronaldo de Lima 15
3. Gerd Müller 14
4. Just Fontaine 13
5. Lionel Messi 13
6. Pele 12
7. Kylian Mbappé 12