Dar es Salaam. Baadhi ya wanasiasa na wadau wa demokrasia wamewataka Watanzania kuthamini umuhimu wa Taifa kwa kuepuka kufanya vitendo vitakavyoharibu taswira na mustakabali wa nchi.
Mbali na hilo, wamesisitiza umuhimu wa kuwepo wa Katiba mpya huku wakiitaka Serikali kusimamia kwa ufanisi haki za binadamu ili kuondokana na matukio ya watu kutekwa au kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Wameeleza hayo leo Jumatano Juni 3, 2026 wakati uzinduzi wa makala maalumu kuhusu matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025, yaliyoandaliwa na mwandishi wa habari wa Nigeria, David Hundeyin.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani ya Oktoba, jumla ya watu 518 kati yao wanaume 490 na wanawake 28 walifariki dunia kutokana na ghasia zilizotokea Oktoba 29, 2025
Akizungumza baada ya makala hayo kuoneshwa yakiwa na maudhui kuhusu kilichojiri Oktoba 29, 2025 katika mkutano huo, Katibu wa Chama cha NRA, Almas Kisbya amewataka Watanzania kuthamini utaifa, maliasili na misingi iliyowekwa.
Kisabya amesema baada ya kuona makala hayo, amegundua namna nguvu vyombo vya habari vya nje ya Tanzania vilivyosaidia yaliyotokea Oktoba 29, 2025 kwa kuleta taarifa zisizo sahihi.
“Watanzania tunaamini hatuna baba wala mjomba atakayeweza kusimama kwa ajili yetu, lazima sisi wenyewe tuamini kwamba jambo likifanya ndani ya nchi ni kwa sababu ya manufaa yetu.”
“Kama tunahitaji mabadiliko, basi tufuate utaratibu uliowekwa si kwa kukurupuka, sio kudanganywa na watu nje kwamba tunaweza kuamka asubuhi na kupata Katiba Mpya,” amesema Kisabya.
Mwanasiasa huyo, amesema watu wanafanya siasa ili kutatua changamoto za Watanzania si kuchonganisha watu bali kuwafanya wawe kitu kimoja.
“Lazima tufanye mambo ambayo tunajua kesho, tutakuwa na uhakika wa Taifa letu,” amesema Kisabya aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe Hamad Rashid amesema kupitia makala hayo amejifunza kuhusu umuhimu wa Watanzania kujitambua na kulinda maliasili, uhuru na umoja uliopo.
“Pamoja na upungufu uliopo, haiwezekani hata siku moja mgeni akatusaidia bali atakuja kwa lengo la kututawala na kuchukua rasilimali. Upungufu utakuwepo, lakini tunahitaji kulinda uhuru na umoja wetu,” amesema Hamad.
Katika hatua nyingine, Hamad aliyewahi kuwa mbunge wa Wawi kisiwani Pemba amesema ni wakati mwafaka kwa Serikali kuwaeleza Watanzania kuhusu utaratibu wa upatikanaji wa Katiba mpya.
Mbali na hilo, Hamad amegusia suala la haki za binadamu akitaka Serikali izingatie kwa kurudi katika mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa kupitia Tume au kamati zilizoundwa ya namna ya kushughulikia jambo hilo.
Mchambuzi wa siasa, Fahamy Matsawili amesema vyama vya siasa, taasisi za kidini, wanaharakati na asasi za kiraia kwa pamoja zinawajibu wa kuhakikisha umoja wa kitaifa unaimarika nchini, akirejea sababu na vichocheo vilivyotajwa na Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Oktoba 29.
Naye, mwandishi wa makala hayo kutoka Nigeria, Hundeyin ameeleza umuhimu wa Watanzania kulilinda Taifa lao, akisema kilichotokea kimewahi kujitokeza katika mataifa ya Nigeria na Ghana kwa nyakati tofauti na kusababisha madhara mbalimbali.
Hundeyin ameitaja Tanzania kama nchi inayoimarika kiuchumi na kidiplomasia hivyo si watu wote watapenda kuona mafanikio hayo au kufikia hadhi hiyo, hivyo lazima ijilinde na siasa au mikakati ya kimataifa inayolenga kuchafua taswira ya Taifa hili.