Kombe la Dunia la FIFA 2026 linaweza kushuhudia kizazi kipya cha wanasoka wanaofuata nyayo za baba zao. Baadhi ya nyota wanaotarajiwa kushiriki mashindano hayo ni watoto wa wachezaji waliowahi kung’ara katika fainali za Kombe la Dunia miaka iliyopita.

Imechapishwa:

Dakika 6 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Na Hannah Nalianya

Hadi sasa, jumla ya jozi 27 za baba na mwana zimewahi kushiriki Kombe la Dunia. Familia za Mazinho na Thiago, Alonso, Djorkaeff, Forlan, Maldini, Reyna, Schmeichel na Thuram ni baadhi ya zilizoweka historia hiyo. Mwaka 2026, sura mpya zinaweza kuongezwa kwenye orodha hiyo.

Tunawaangazia wachezaji hao:

GREGG BERHALTER NA SEBASTIAN BERHALTER (MAREKANI)

Baba: Gregg Berhalter

Alishiriki fainali mbili za koùbe la Dunia na kucheza mechi mbili, ambapo kati ya hizo hakuwahi kufunga. Berhalter alikuwa nguzo muhimu katika safu ya ulinzi ya Marekani kwenye Kombe la Dunia 2002 nchini Korea Kusini na Japan.

Aliisaidia timu yake kuiondoa Mexico katika hatua ya 16 bora kabla ya Marekani kutolewa na Ujerumani kwa bao 1-0 katika robo fainali. Baadaye alishiriki Kombe la Dunia 2006 na pia aliifundisha Marekani kwenye Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

Mtoto: Sebastian Berhalter

Huyu anacheza nafasi ya kiungo, aliingia katika kikosi cha timu ya taifa mwaka jana na kuvutia kwa kiwango chake.

Alifunga katika ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Uruguay na kuendelea kung’ara akiwa Vancouver Whitecaps, jambo lililomweka katika mipango ya kocha Mauricio Pochettino kuelekea Kombe la Dunia 2026.

SERGIO CONCEICAO NA FRANCISCO CONCEICAO (URENO)

Baba: Sergio Conceicao

Kombe la Dunia: Mara 1

Mechi: 3

Mabao: 0

Sergio Conceicao alikuwa sehemu ya kikosi cha Ureno kilichoshiriki Kombe la Dunia 2002. Alisaidia timu hiyo kuifunga Poland mabao 4-0 katika hatua ya makundi, lakini Ureno ilishindwa kuvuka hatua ya kwanza ya mashindano hayo.

Mtoto: Francisco Conceicao

Anacheza nafasi ya mshambuliaji wa pembeni na ana urefu wa mita 1.65 amekuwa mmoja wa nyota wa kizazi kipya cha Ureno.

Alifunga bao la ushindi dhidi ya Czechia katika mechi ya ufunguzi ya Mashindano ya Mataifa ya Ulaya 2024 na baadaye akafunga tena katika ushindi dhidi ya Ujerumani kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mataifa mwezi Juni.

LEE EULYONG NA LEE TAESEOK (KOREA KUSINI)

Baba: Lee Eulyong

Kombe la Dunia: Mara 2

Mechi: 6

Mabao: 1

Kiungo huyo anakumbukwa kwa bao lake maridadi la mpira wa adhabu katika mechi ya kuwania nafasi ya tatu kwenye Kombe la Dunia 2002. Pia aliiwakilisha Korea Kusini katika Kombe la Dunia 2006.

Mtoto: Lee Taeseok

Beki huyo wa kushoto mwenye umri wa miaka 23 amekuwa katika kiwango bora. Alifunga bao la kipekee katika ushindi wa Korea Kusini dhidi ya Ghana mwezi Novemba na pia ameonyesha uwezo mkubwa wa kushambulia akiwa Austria Vienna.

BRYAN GUNN NA ANGUS GUNN (SCOTLAND)

Baba: Bryan Gunn

Kombe la Dunia: Mara 1

Mechi: 0

Bryan Gunn alikuwa kipa wa tatu wa Scotland kwenye Kombe la Dunia 1990 nchini Italia nyuma ya Jim Leighton na Andy Goram, lakini hakupata nafasi ya kucheza.

Mtoto: Angus Gunn

Baada ya kuiwakilisha England katika ngazi za vijana, Angus alibadili utii wake wa kimataifa na kuichezea Scotland mwaka 2023. Tangu wakati huo amekuwa chaguo la kwanza golini kwa taifa hilo. Baada ya kupona jeraha la goti mwezi Desemba, alicheza dakika 45 pekee akiwa Nottingham Forest.

ALFIE HALAAND NA ERLING HAALAND (Norway)

Baba: Alfie Haaland

Kombe la Dunia: Mara 1

Mechi: 2

Mabao: 0

Alfie Haaland alicheza kama beki wa kulia katika Kombe la Dunia 1994, mashindano ambayo yalikuwa ya kwanza kwa Norway baada ya miaka 56. Hata hivyo, Norway iliondolewa kwa tofauti ya mabao ya kufunga licha ya kuwa na pointi sawa na timu nyingine katika kundi lake.

Mtoto: Erling Haaland

Norway inarejea kwenye Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya miaka 28 na itakuwa pamoja na Ufaransa na Senegal katika Kundi I. Ikiwa na Erling Haaland, mmoja wa washambuliaji hatari zaidi duniani, taifa hilo lina matumaini makubwa ya kufanya vizuri.

Je, wajua?

Mnamo Oktoba 2025, Haaland alikua mchezaji wa sita tu katika historia kufikisha mabao 50 ya kimataifa katika mechi chini ya 50. Pia alikuwa wa kwanza kufanya hivyo katika kipindi cha miaka 53.

PATRICK KLUIVERT NA JUSTIN KLUIVERT Kluivert (Uholanzi)

Baba: Patrick Kluivert

Kombe la Dunia: Mara 1

Mechi: 4

Mabao: 2

Patrick Kluivert alitolewa kwa kadi nyekundu katika mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia dhidi ya Ubelgiji mwaka 1998. Alirejea na kufunga katika ushindi wa robo fainali dhidi ya Argentina na baadaye akafunga tena dhidi ya Brazil katika nusu fainali, ingawa Uholanzi iliondolewa kwa mikwaju ya penalti.

Mtoto: Justin Kluivert

Justin alikuwa na msimu bora akiwa Bournemouth mwaka 2024/25, jambo lililomfanya kuwa chaguo la kudumu katika kikosi cha Uholanzi. Licha ya kusumbuliwa na majeraha msimu uliopita, Ronald Koeman alimjumuisha katika kikosi cha mashindano ya Amerika Kaskazini.

DIEGO SIMEONE NA GIULIANO SIMOENE (Argentina)

Baba: Diego Simeone

Kombe la Dunia: Mara 3

Mechi: 11

Mabao: 0

Diego Simeone alikuwa mmoja wa viongozi wa Argentina katika Kombe la Dunia mara tatu. Katika Kombe la Dunia 1998, alihusika katika tukio maarufu lililosababisha David Beckham kutolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo wa hatua ya 16 bora kati ya Argentina na England.

Mtoto: Giuliano Simeone

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 amekuwa muhimu katika kikosi cha Atletico Madrid kinachonolewa na baba yake. Pia ameendelea kupata nafasi katika timu ya taifa ya Argentina na alifunga katika ushindi mkubwa wa mabao 4-1 dhidi ya Brazil mwaka 2025.

Je, wajua?

Diego aliporejea kuishi Madrid mwaka 2011, aliendelea kula chakula pamoja na wanawe watatu kupitia simu za video huku kila mmoja akifuatilia ndoto zake za kuwa mwanasoka.

ERIK THORSTVEDT NA KRISTIAN THORSTVEDT (Norway)

Baba: Erik Thorstvedt

Kombe la Dunia: Mara 1

Mechi: 3

Mabao: 0

Kipa huyo aliruhusu bao moja pekee katika mechi tatu za Norway kwenye Kombe la Dunia 1994. Hata hivyo, timu hiyo iliondolewa katika hatua ya makundi licha ya kukusanya pointi nne.

Mtoto: Kristian Thorstvedt

Kiungo huyo alikuwa na msimu mzuri akiwa Sassuolo mwaka 2025/26. Pia alichangia Norway kuifunga Italia mabao 4-1 na kufuzu Kombe la Dunia.

Je, wajua?

Erik Thorstvedt na Alfie Haaland walicheza pamoja katika Kombe la Dunia 1994. Kristian Thorstvedt na Erling Haaland wanaweza kuwa watoto wa kwanza wa wachezaji wenza wa Kombe la Dunia kucheza pamoja katika mashindano hayo.

ZINEDINE ZIDANE NA LUCA ZIDANE (Algeria)

Baba: Zinedine Zidane

Kombe la Dunia: Mara 3

Mechi: 12

Mabao: 5

Zinedine Zidane ni mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kucheza Kombe la Dunia. Aliiongoza Ufaransa kutwaa ubingwa mwaka 1998 na kufika fainali tena mwaka 2006.

Mtoto: Luca Zidane

Luca, ambaye ni mtoto wa pili kati ya wana wanne wa Zidane wanaocheza soka, aliwahi kuichezea Ufaransa katika ngazi za vijana kabla ya kubadili utii wake wa kimataifa na kuichezea Algeria. Kipa huyo wa Granada alicheza mechi yake ya kwanza kwa Algeria mwezi Oktoba 2025.

Je, wajua?

Katika robo fainali ya Kombe la Dunia 2006 dhidi ya Brazil, Zidane alifanikiwa kupiga chenga zote 11 alizojaribu, jambo linalotajwa kama moja ya maonyesho bora kabisa katika historia ya mashindano hayo.

Kombe la Dunia 2026 kinaweza kuwa jukwaa la kizazi kipya kuendeleza urithi wa familia zao. Kwa baadhi yao, itakuwa nafasi ya kuthibitisha kuwa wanaweza kuandika historia yao wenyewe, huku wakifuata nyayo za baba zao waliowahi kung’ara katika mashindano hayo makubwa zaidi duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *