
Watetezi wa haki za binadamu wamekitaka Chama cha Kitaifa cha Mpira wa Kikapu cha Marekani (NBA) kukomesha ushirikiano wake na Umoja wa Falme za Kiarabuu (UAE), wakisema uhusiano wa ligi hiyo na Abu Dhabi unaikingia kifua nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi kutokana na kulaaniwa vikali kwa kuhusika kwake katika vita ndani nchini Sudan.
Watetezi hao wa haki za binadamu wamejiunga na mbunge wa Chama cha Democratic, James Patrick McGovern, katika kuihimiza NBA kufikiria upya uhusiano wake na UAE.
Kampeni hiyo inakuja huku Sudan ikiendelea kukabiliana na kile ambacho mashirika ya kutetea haki za binadamu yanakielezea kama mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi na wa binadamu unaoendelea kwa sasa duniani.
Abu Dhabi imekuwa ikitoa msaada wa kifedha, zana na mafunzo kwa kile kinachoitwa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), kundi la wanamgambo ambalo limefanya unyanyasaji mkubwa dhidi ya raia katika kipindi chote cha vita vya ndani nchini Sudan.
McGovern, mwenyekiti mwenza wa Tume ya Haki za Binadamu ya Tom Lantos, amesema ushirikiano wa NBA na UAE unaibua wasiwasi mkubwa wa kimaadili.
Amesema kwamba shughuli za kibiashara za ligi ya NBA katika nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi yumkini zikasaidia kuboresha taswira ya serikali inayokabiliwa na ukosoaji mkubwa wa kimataifa kwa kuchangia ukatili nchini Sudan.
“Mashabiki wanapaswa kujua kwamba mchezo wanaoufurahia unachochea uhalifu dhidi ya ubinadamu. Wanapaswa kujua kwamba NBA inawekeza huko UAE, na UAE yenyewe inawekeza katika ukatili nchini Sudan,” amesema McGovern.
Awali, Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch liliripoti kwamba wapiganaji mamluki kutoka Colombia wanapewa mafunzo katika kambi za kijeshi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na kisha wanapelekwa Sudan ili kuwasaidia waasi wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
Shirika hilo limewataka “washirika wa UAE, wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika” kuwataka viongozi wa Imarati kuacha mara moja kutoa silaha, zana, wapiganaji na aina nyingine za misaada kwa RSF.