
Johannesburg (AFP) – Polisi wa Afrika Kusini imesema siku ya Jumanne kuwa raia wawili wa Msumbiji waliuawa katika vurugu mwishoni mwa wiki lakini imelikataa kuthibitisha tangazo la serikali ya Msumbiji kwamba raia wake watano waliuawa katika “mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni”.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Maandamano dhidi ya raia wa kigeni wasio na vibali yamekuwa yakiongezeka katika wiki za hivi karibuni, na kusababisha Ghana kuwarudisha nyumbani takriban raia wake 300 wiki iliyopita, huku Nigeria pia ikitangaza kuwarejesha nyumbani raia wake.
Ghasia zilizuka katika mji wa kusini mwa pwani wa Mossel Bay siku ya Ijumaa baada ya maandamano madogo dhidi ya wahamiaji haramu wanaoshutumiwa kuchukua kazi kutoka kwa wenyeji, maafisa na ripoti zilisema.
Vibanda kadhaa vilichomwa moto, baadhi yao wakiwa bado ndani yake, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.
“Kwa bahati mbaya, raia saba wa Msumbiji wamefariki, watano kati yao waliuawa katika mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni na wengine wawili kutokana na ajali ya barabarani walipokuwa wakisafiri kwa gari la kibinafsi wakirudi Msumbiji,” ofisi ya vyombo vya habari ya serikali ya Msumbiji ilisema siku ya Jumatatu jioni.
Haya ni mauaji ya kwanza yanayodaiwa kuhusishwa na wimbi jipya la maandamano ya kupinga wahamiaji yanayoikumba Afrika Kusini.
Polisi ya Afrika Kusini ilithibitisha tu kwamba raia wawili wa Msumbiji, wenye umri wa miaka 27 na 43, walifariki baada ya kushambuliwa kufuatia maandamano hayo.
Polisi ya Afrika Kusini ilisema hali hiyo inachunguzwa, ikikikataa kuthibitisha uhusiano na hisia za chuki dhidi ya wageni.
Mwili wa kijana wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 18 ulipatikana na majeraha ya kuchomwa kisu katika eneo hilo siku ya Jumapili, polisi ilisema, ikiongeza kuwa alihusika katika jaribio la wizi.
Watu watano walikamatwa tangu ghasia zilipoanza, watatu kati yao kwa mashtaka yanayohusiana na vurugu na kumiliki mali iliyoibwa, polisi ilisema.
‘Hatuko salama’
Shirka la Utangazaji Afrika kusini la SABC lilisema mvutano huko Mossel Bay ulizuka kutokana na madai kwamba wahamiaji haramu wanaajiriwa na makampuni ya ujenzi.
Takriban vibanda 55 vilichomwa moto, mamlaka ilisema.
“Tulikuwa ndani wakati watu walianza kuchoma nyumba yetu,” raia wa Msumbiji Dolinda Mabunda alisema.
“Nilichukua tu nilichoweza na nikakimbia,” aliongeza.
“Nitarudi (nyumbani) kwa sababu hatuko salama,” mhamiaji anayeitwa Silvino Chauque aliliambia shirika la Utangazaji la SABC, kuwa amepoteza mali zake zote katika machafuko.
Serikali ya Msumbiji ilisema raia 300 wa Msumbiji walirudi nyumbani siku ya Jumamosi.
“Watu 500 wanaosalia wamehifadhiwa katika eneo salama katika jimbo la Western Cape, na mchakato wa kuwarejesha Msumbiji ulianza tangu Juni 1,” ilisema..
Meya wa mji wa Mossel Bay, Dirk Kotze, mwishoni mwa wiki alielezea “wasiwasi mkubwa na kusikitishwa na mashambulizi ya sasa ya chuki dhidi ya wageni ambapo watu wameuawa, nyumba zimechomwa moto na familia zimelazimika kuhama makazi”.
Baada ya shirika moja linaloongozwa na raia kudai kwamba raia wa kigeni wasio na vibali waondoke Afrika Kusini ifikapo Juni 30, kumekuwa na ripoti zamakundi ya ulinzi yanayoangalia nyaraka za raia wa kigeni na kulazimisha biashara ndogo ndogo zinazoendeshwa na wasio Waafrika Kusini kufunga.
Kitendo hicho hakiungwi mkono rasmi na kimekosolewa na mamlaka.
Mwezi uliopita mamia kadhaa ya raia wa kigeni kutoka nchi ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Somalia walitafuta ulinzi katika mji wa bandari wa mashariki wa Durban, wakisema wenyeji walikuwa wakienda nyumba kwa nyumba kuwaambia waondoke ifikapo mwisho wa mwezi.
Nchi kadhaa ikiwemo Kenya, Malawi, Lesotho na Zimbabwe wakati huo huo zimewasihi raia wao nchini Afrika Kusini kuwa waangalifu.
Afrika Kusini imepitia ghasia za chuki dhidi ya wageni katika miaka iliyopita. Ongezeko la hivi karibuni linakuja huku vyama vya siasa vikitafuta uungwaji mkono kabla ya uchaguzi mwezi Novemba.
Mnamo 2008, watu 62 — wakiwemo Waafrika Kusini 21 — waliuawa katika ghasia za kupinga wahamiaji ambazo pia zilisababisha maelfu ya watu kuondoka katika nchi hiyo. Ghasia zingine zilifuata mwaka 2015 na 2016.
© 2026 AFP