Kisha hicho kinaelezwa na Dkt. Marie-Rosaline Belizaire, Mkurugenzi wa Dharura wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO, Kanda ya Afrika wakati akihojiwa kwa njia ya video kutoka DRC na Idhaa ya Kifaransa ya Umoja wa Mataifa.

“Timu ya wahudumu wa afya ilitumwa kusaidia familia moja baada ya ndugu yao aliyefariki kuthibitika kuwa alikuwa na Ebola. Lengo lao lilikuwa kufanya mazishi salama na yenye heshima, hatua muhimu katika kuzuia maambukizi zaidi ya virusi hivyo. Hata hivyo, wanafamilia walikataa kukubali matokeo ya uchunguzi na wakaanza kuwa na uhasama,” amesema Dkt. Belizaire.

Amesema hali ilizidi kuwa mbaya wakati baadhi ya wakazi wa eneo hilo walipotishia kuwaita waasi wenye silaha iwapo wahudumu hao wangebaki katika eneo hilo. Kwa kuhofia usalama wao, timu ya wataalamu wa afya ililazimika kuondoka haraka.

“Baada ya timu hiyo kuondoka, wanajamii waliuchukua mwili wa marehemu aliyekufa kwa Ebola na kuusafirisha wenyewe, jambo lililowaweka watu wengi katika hatari ya kuambukizwa virusi hivyo,” amefafanua Afisa huyo akiongeza kuwa, “kwa wahudumu wa afya, matukio kama haya yanakatisha tamaa sana. Mara nyingi hulazimika kuchagua kati ya usalama wao binafsi na wajibu wao wa kulinda afya ya umma.”

Tukio hili linakuja wakati hadi Juni 3, DRC imerekodi wagonjwa 381 waliothibitishwa kuwa na Ebola na kati yao hao 64 wamekufa huku Uganda jirani ikiripoti wagonjwa 15 waliothibitishwa na mtu mmoja anayeshukiwa kuwa na Ebola amekufa.

Dkt. Belizaire amesema ingawa uwezo wa upimaji umeongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka vipimo 40 kwa siku mwanzoni mwa mlipuko hadi vipimo 800 kwa siku hivi sasa, upinzani kutoka kwa baadhi ya wananchi unaendelea kuwa kikwazo kikubwa katika kudhibiti ugonjwa huo.

Kwa nini jamii haziamini mamlaka za afya?

Kwa mujibu wa Dkt. Belizaire, kutokuaminiana huko kunatokana na imani za kitamaduni, taarifa potofu na kufanana kwa dalili za Ebola na magonjwa ya kawaida kama malaria.

Katika baadhi ya jamii, magonjwa na vifo huhusishwa na uchawi au sumu badala ya magonjwa ya kuambukiza. Hadithi za kijamii na mila mbalimbali huimarisha mitazamo hiyo na kufanya iwe vigumu kwa wananchi kukubali maelezo ya kisayansi.

“Baadhi ya viongozi wa jamii wamefikia hatua ya kuhoji kama aina ya Ebola ya Bundibugyo ipo kweli. Kutokana na hali hiyo, wahudumu wa afya wanakabiliwa na changamoto mbili kwa wakati mmoja: kutibu wagonjwa na wakati huo huo kushughulikia hofu na imani potofu zilizojengeka kwa muda mrefu,” amesema.

Afisa huyo amesisitiza kuwa hatulengi kubadilisha utamaduni wa watu bali wanajaribu kuunganisha sayansi ndani ya mfumo wao wa kitamaduni.

Wahudumu wa afya waliopona Ebola waendelea kutibu wagonjwa

Hatari zinazowakabili wahudumu wa afya haziishii kwenye vitisho na vitendo vya kutisha pekee. Wahudumu hao pia wanaendelea kuwa miongoni mwa wanaoambukizwa virusi hivyo.

Kati ya watu saba waliopona Ebola katika mlipuko huu, sita ni wahudumu wa afya. Wengi wao waliambukizwa walipokuwa wakiwahudumia wagonjwa. Licha ya hatari hizo, wengi wao wanaendelea kujitolea kuhudumia jamii zao.

Dkt. Belizaire amekumbuka kukutana na mhudumu mmoja wa afya aliyeambukizwa alipokuwa akiwatibu wagonjwa. Baada ya kupona, mwanamke huyo alieleza dhamira yake ya kuendelea na kazi hiyo.

“Amesema hataacha kazi yake,” amesimulia Dkt. Belizaire. “Ameamini  alizaliwa kuwahudumia wengine, na hilo ndilo ataendelea kufanya.”

Kujitolea kwa namna hiyo kunaonesha kiwango kikubwa cha kujitoa mhanga kinachofanywa na wahudumu wa afya wakati wa dharura za afya ya umma.

Nini kinapaswa kufanyika?

Kuimarisha ushirikishwaji wa jamii.

Viongozi wa mitaa, vikundi vya wanawake, mashirika ya vijana, viongozi wa dini na vyama vya waendesha bodaboda wanapaswa kushirikishwa katika kampeni za uelimishaji. Mara nyingi sauti zinazotoka ndani ya jamii huaminika zaidi kuliko maafisa kutoka nje.

Kushirikiana na waganga wa jadi.

Badala ya kuwatenga, mamlaka za afya zinapaswa kuendelea kushirikiana nao kwa kuwapatia vifaa vya kujikinga na mafunzo ya kutambua dalili za Ebola na kuwapeleka wagonjwa katika vituo vya afya.

Kuboresha mawasiliano kuhusu hatari.

Taarifa kuhusu namna Ebola inavyoambukizwa, dalili zake, upimaji na matibabu zinapaswa kutolewa kwa lugha za wenyeji na kupitia njia zinazokubalika kitamaduni.

Kulinda wahudumu wa afya. 

Tathmini za usalama na juhudi za upatanishi wa kijamii zinapaswa kuambatana na operesheni za kukabiliana na mlipuko katika maeneo yenye hatari kubwa ili kupunguza vitisho dhidi ya timu za afya.

Kukuza simulizi za walionusurika.

Kushirikisha hadithi za watu waliopona Ebola kunaweza kuonyesha kuwa matibabu ya mapema yanaokoa maisha na kusaidia kuondoa dhana kwamba maambukizi ya Ebola ni hukumu ya kifo.

Kuongeza ushiriki wa jamii.

Wananchi wanapaswa kushirikishwa katika maamuzi yanayohusu hatua za kukabiliana na mlipuko, ikiwemo taratibu za mazishi salama na ufuatiliaji wa waliokutana na wagonjwa.

Imani ndiyo silaha muhimu zaidi

Wakati wanasayansi wanaendelea kufanya kazi ya kutengeneza chanjo na matibabu ya aina ya Bundibugyo ya Ebola, Dkt. Belizaire amesisitiza kuwa hakuna mafanikio ya kitabibu yanayoweza kuchukua nafasi ya ushirikiano wa jamii.

Wagonjwa wanaotafuta matibabu mapema wana nafasi kubwa zaidi ya kupona, na mamlaka za afya zimefanikiwa kupunguza muda wa kusubiri majibu ya vipimo hadi chini ya saa 48.

Hata hivyo, kwa muda wote ambao hofu na kutokuaminiana vitaendelea kuwepo, wahudumu wa afya wataendelea kukabiliwa na upinzani, vitisho na vurugu.

Mlipuko wa Ebola nchini DRC ambao ni wa 17 unaonesha kuwa mapambano dhidi ya dharura za afya ya umma hayafanywi tu katika maabara na hospitali. Pia hupiganwa ndani ya jamii, ambapo imani inaweza kuwa tofauti kati ya kudhibiti ugonjwa au kuruhusu kuenea kwake zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *