
Seneta wa kujitegemea kutoka Vermont, Bernie Sanders, ametangaza kwamba atapinga sheria inayochunguzwa bungeni ambayo itaongeza ushawishi wa Israel katika taasisi za kijeshi na viwanda vya Marekani.
“Netanyahu anajua Wamarekani wamechoka kufadhili vita vya Israel. Kwa hivyo sasa anafanya kazi na Bunge kuficha misaada ya kijeshi ndani ya mikataba ya uzalishaji wa pamoja ya Pentagon,” amesema seneta huyo wa Vermont katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii mapema leo Jumapili.
Sanders ameonya kwamba pendekezo hilo, lililowasilishwa na Netanyahu kama kupunguzwa kwa misaada ya Marekani, kivitendo litasababisha pesa nyingi zaidi za walipa kodi wa Marekani kuelekezwa Israel.
Amesisitiza: “Hili halitatokea!”
Inasemekana kwamba kifungu hicho, ambacho kimejumuishwa katika Sheria ya Idhini ya Ulinzi wa Kitaifa ya Marekani, pia kimekabiliwa na upinzani kutoka kwa wabunge wengine wawili, Ro Khanna na Thomas Massie.
Ingawa pendekezo hilo bado halijapigiwa kura katika Kongresi, ikiwa litaidhinishwa, litaiweka Marekani katika matatizo mengi ya kijeshi na kisiasa ya Israel.