Wekesa mwenye umri wa miaka 25, ameeleza nia yake, alipotembelea ofisi za Umoja wa Mataifa nchini Kenya, Amwezi Aprili mwaka huu. Katika mahojiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira, UNEP, Wekesa amesema ziara hiyo imejikita kufanya mazungumzo ya namna gani michezo na mazingira vinaweza kufanya kazi pamoja.

Akiwa uwanjani, amepata sifa za kimataifa akiichezea timu ya raga iitwayo Kenya Sevens na kutimiza ndoto yake ya kushiriki Olimpiki. Hivi sasa Wekesa ameanzisha taasisi ya mazingira, Play Green (yaani cheza kwa kujali mazingira), inayolenga kuwahimiza wachezaji, mashabiki, na wadau wa michezo kuzingatia uendelevu wa mazingira.

“Play Green inajaribu kuleta uhusiano uliopo kati ya michezo na mazingira na katika Play Green inaangazia sekta nne sana sana katika maisha yetu. Moja ikiwaupandaji wa miti, kutokomezachupa za plastiki katika michezo na zile jamii ambazo zinaishi karibu na watu wanaojihusisha na michezo halafu pia kuna urejelezaji na mwishowe ni kutoa elimu ya mazingira kwa kupitia michezo kwa wanamichezo na wasio wanamichezo.”

Msukumo wa kuhifadhi mazingira ulikuja akiwa uwanjani akicheza raga na watoto nchini Kenya, upepo mkali na ugumu wa kukimbia uwanjani vilimwonesha madhara ya moja kwa moja ya mabadiliko ya tabianchi kwenye michezo na kuamua kuchukua hatua, wachezaji wenzake sasa wanamuunga mkono.

“Wachezaji tunaocheza nao katika raga wameniunga mkono sana, wananisaidia katika taasisi yangu na wanapenda pia kujua zaidi na kutumia majina yao kufikisha huu ujumbe wa kulinda dunia yetu”

© UNEP Kevin Wekesa anafurahia utambulisho wake kama mchezaji nyota wa raga na mwanamazingira.

Wekesa ambaye pia ni miongoni mwa washindi wa Tuzo za Shirikisho la Kimataifa la Olimpiki, IOC za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi za mwaka 2025, anatoa wito kwa dunia na vijana wadogo kama yeye.

“Kwa sasa sio lazima ufanye vitu kwa kiwango kikubwa, unaweza ukafanya vitu polepole na mwishowe vinajijumlisha kuwa kitu kikubwa, kama wewe mwenyewe ukianza pekeyako na pia mwingine mmoja ama wawili wakufuate, watatu, wanne, mwishowe litakuwa kundi kubwa sana na hapo utaweza kuisaidia dunia yetu”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *