
Kocha wa zamani wa Simba, Didier Gomes Da Rosa, ametangazwa kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Sierra Leone.
Jukumu kubwa ambalo kocha huyo amepewa ni kuiongoza Sierra Leone kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 zitakazofanyika Kenya, Uganda na Tanzania.
Mfaransa huyo anaziba nafasi iliyoachwa wazi na Mohamed Kallon ambaye alitimuliwa katika nafasi hiyo hivi karibuni.
Da Rosa aliyewahi kuipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuiongoza kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2020/2021, amewahi pia kuzinoa klabu za Horoya, CS Consfantine, Al Wehdat, Al Merreikh, Ismaily, Coton Sports, Rayon Sports na timu ya Taifa ya Botswana.
Akizungumzia uteuzi huo, Da Rosa amesema kuwa atahakikisha anawapa furaha mashabiki wa soka nchini humo.
“Ni heshima kwangu kuhudumu kama Kocha wa timu ya taifa ya Sierra Leone. Lengo letu liko wazi. Fanya kazi kwa bidii, cheza kwa fahari ya taifa lako na hamasisha taifa.
“Nawashukuru Rais wa Chama cha Soka Sierra Leone, wajumbe wa bodi na mamlaka zilizopitisha jina langu,” amesema Gomes.