
Anold Kayanda ameufuatilia ujumbe wa GuteAkizungumza kwa njia ya video katika ujumbe wake wa Siku ya Kimataifa ya Bahari, Bwana Guterres amesema bahari ni msingi wa maisha na maendeleo duniani, lakini zimekuwa zikikabiliwa na shinikizo linalozidi uwezo wake wa kustahimili.
“Bahari inaongoza tabianchi yetu, inalinda mifumo ya ikolojia na uchumi, na inalisha mabilioni ya watu duniani,” anasema Guterres na kuongeza kuwa, “bahari ipo kwenye zahma kubwa na tunaishinikiza kupita uwezo wake.”
Guterres amerejelea Ripoti ya Tatu ya Tathmini ya Bahari Duniani iliyozinduliwa leo, ambayo imebainisha kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi, uvuvi uliokithiri, kupotea kwa bionuwai na uchafuzi wa bahari.
Katibu Mkuu Guterres amesisitiza akisema, “hatuwezi kuendelea kuichukulia bahari kama kitu kisicho na ukomo,” akihimiza kujengwa kwa uhusiano mpya na bahari unaozingatia sayansi, unaoongozwa na sheria za kimataifa na unaojengwa juu ya wajibu wa pamoja wa mataifa, sekta mbalimbali na vizazi vyote.
Ametaja mafanikio ya Mkutano wa Tatu wa Bahari wa Umoja wa Mataifa uliofanyika mwaka jana pamoja na kuanza kutekelezwa kwa Makubaliano ya Baionuai ya Bahari katika maeneo yaliyo nje ya mamlaka ya kitaifa mwaka huu kama ushahidi kwamba ushirikiano wa kimataifa unaweza kuleta matokeo.
Anasema, “hatua za pamoja za kimataifa zinawezekana na ni za lazima.”
Katika hitimisho la ujumbe wake wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewataka viongozi wa dunia, sekta binafsi na wananchi kuchukua hatua kwa haraka ili kulinda bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Anasema, “katika Siku hii ya Kimataifa ya Bahari, hebu tuchukue hatua kwa nia thabiti na kutatua mahitaji ya wakati huu.”
Hakika yanayosemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa yanaendana na aliyoyasema Mwenyekiti wa Tume ya Kiserikali ya masuala ya Bahari ya shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO (IOC) kwa bara la Afrika na Nchi za Visiwa vinavyokaribia bara hilo (IOCAFRICA) Balozi Hellen Gichuhi alipozungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa huko Nairobi nchini Kenya.