Idadi ya visa vilivyothibitishwa vya ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imefikia 515, vikiwemo vifo 91, huku mamlaka za afya zikionya kuwa maambukizi bado yanaendelea na huenda visa vikazidi kuongezeka ikiwa hatua za udhibiti hazitaimarishwa haraka.

Taarifa hiyo, iliyotolewa Jumapili na Wizara ya Afya ya DRC, imesema wagonjwa watatu zaidi wametangazwa kupona, na hivyo kufanya idadi ya waliopona kufikia 12 kufikia tarehe 6 Juni.

Ripoti hiyo pia ilieleza kuwa visa 117 vinashukiwa kuwa vya Ebola, huku wagonjwa 283 wakiendelea kuwa katika vituo vya uangalizi maalum au wakiwa hospitalini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, idadi kubwa ya wagonjwa waliothibitishwa walionyesha dalili kati ya Mei 14 na Mei 23, hali inayodokeza uwezekano wa maambukizi makubwa kutoka chanzo kimoja kinachoshukiwa, huku kilele cha visa kikiripotiwa Mei 18.

Ripoti hiyo iliongeza kuwa kundi jingine la wagonjwa waliothibitishwa lilianza kuonyesha dalili kati ya Mei 25 na Juni 3, jambo linaloashiria kuendelea kwa kuenea kwa ugonjwa huo na huenda likawa chanzo muhimu cha maambukizi zaidi.

Taarifa hiyo imesema: “Iwapo hatua stahiki hazitawekwa haraka sana, kuna uwezekano wa kuongezeka zaidi kwa visa.”

Hata hivyo, juhudi za kukabiliana na mlipuko huo bado zinakabiliwa na changamoto kadhaa, zikiwemo ufuatiliaji dhaifu wa watu waliokutana na wagonjwa, upinzani kutoka kwa baadhi ya jamii kuhusu uchunguzi wa miili baada ya vifo, uhaba wa uwezo katika vituo maalum vya matibabu ya Ebola, pamoja na upungufu wa vifaa vya kudhibiti maambukizi na ufadhili mdogo.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa kiwango cha ufuatiliaji wa watu waliokutana na wagonjwa katika majimbo matatu yaliyoathirika kimefikia asilimia 50.3 pekee, kiwango kilicho chini sana ya lengo la asilimia 95.

Aidha, uwezo wa maabara unaendelea kuwa chini ya shinikizo, huku matokeo ya vipimo 193 yakiwa bado hayajatolewa kutokana na uhaba wa kemikali za maabara (reagents) katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Mlipuko wa sasa wa Ebola, unaosababishwa na aina ya Bundibugyo ya virusi vya Ebola, ulitangazwa rasmi na Wizara ya Afya tarehe 15 Mei.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *