
Arusha. Mkoa wa Arusha umeanza utekelezaji wa mpango wa kuwaondoa watoto 750 wanaoishi na kufanya kazi mitaani kwa kuwaunganisha tena na familia zao au mifumo mingine salama ya malezi, ili waweze kupata huduma stahiki za malezi, elimu, afya na ulinzi.
Mpango huo unatekelezwa na shirika la kuhudumia watoto ‘SOS Children’s Villages’ tawi la Tanzania kwa kushirikiano na Serikali, kwa lengo la kupunguza idadi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kwa kuwapatia fursa ya maisha bora kupitia mazingira salama ya makuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari June 9,2026 jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Mkurugenzi wa SOS Children’s Villages Tanzania, Thomas Kipingili, amesema mradi huo unalenga kuwaunganisha watoto hao na familia zao au mifumo rasmi pamoja na kuimarisha uwezo wa familia na jamii katika kuwalea na kuwalinda watoto.
Amesema mradi huo unafuatia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita katika mikoa inayoongoza kuwa na watoto wa mitaani ya Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza.
“Katika mikoa hiyo watoto zaidi ya 1,901 waliokolewa kutoka mazingira ya mtaani na 1,017 kati yao kuunganishwa tena na familia zao”.
“Aidha, zaidi ya familia 1,067 ziliwezeshwa kuimarisha uwezo wao wa kutoa malezi bora kwa watoto kupitia huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi”.
Kipingili amesema mradi huo unalenga pia kuimarisha mifumo ya Serikali na jamii katika ulinzi wa mtoto ili kuhakikisha watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wanatambuliwa mapema na kupata huduma stahiki kwa mujibu wa sheria na sera za nchi.
“Mafanikio tuliyoyapata yanaonyesha kuwa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani wanaweza kurejeshewa matumaini na kupata maisha bora wanapopata msaada sahihi kutoka kwa familia, jamii na taasisi mbalimbali,” amesema.
Kwa mujibu wa Kipingili, katika awamu mpya ya utekelezaji inayoanza leo, jumla ya watoto 4,200 watanufaika na mradi huo katika maeneo mbalimbali nchini, huku watoto 750 wakifikiwa katika Mkoa wa Arusha.
“Mradi huu utatekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na Halmashauri ya Wilaya ya Meru”.
Akizindua mradi huo Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amesema mkoa huo umeanza hatua za kukabiliana na changamoto ya watoto wa mitaani ikiwemo kufanya sensa ya kuwatambua.
“Amesema katika sensa hiyo kwa Arusha mjini pekee Kuna jumla ya watoto 631 wanaishi na kufanya kazi mitaani, huku 94 kati yao wakilala mitaani”.
Amesema watoto hao hupatikana zaidi katika Kituo Kikuu cha Mabasi, Kituo cha Daladala, Soko la Kilombero, Soko Kuu na Mianzini ambayo ni maeneo yanayovutia shughuli nyingi za kiuchumi.
Mkude amesema mkoa una matarajio ya kuwa mfano wa kuigwa katika kushughulikia changamoto hiyo ifikapo mwaka 2029.
“Tunatarajia kuwaondoa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani na kuwaunganisha na huduma muhimu ikiwemo malezi, malazi, elimu, afya na mafunzo ya stadi za maisha,” amesema.
Amesema ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, mashirika ya maendeleo, viongozi wa jamii na wadau wengine wa ulinzi wa mtoto ndio itasaidia kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.