Hatimaye duru mpya ya vita kati ya utawala wa Kizayuni na Iran ilianza Jumapili, kufuatia utawala huo kuishambulia Lebanon mara kwa mara; na ingawa ilikuwa fupi, lakini ilikuwa na ujumbe muhimu.

Ujumbe wa kwanza wa vita hivyo vipya na vya muda mfupi ni kwamba, utawala wa Kizayuni unaendelea kuwa na nafasi haribifu na ya kuvuruga mazungumzo kati ya Iran na Marekani. Utawala wa Kizayuni, ambao ni kikwazo kikubwa kwa makubaliano yoyote kati ya Iran na Marekani na kutaka kuendeleza vita dhidi ya Iran, kwa mashambulizi ya mara kwa mara katika maeneo ya kusini mwa Lebanon na Beirut, umeipelekea Iran kuanzisha vita hivyo kwa ajili ya kuitetea Hizbullah na na wakati huo huo kukabiliana na ukiukaji vita wa mara kwa mara unaofanywa na utawala huo ghasibu. Hii ni katika hali ambayo mazungumzo kati ya Iran na Marekani yanaendelea, na hata Rais wa Marekani Donald Trump amedai kuwa kuna uwezekano mkubwa wa makubaliano ya Tehran na Washington kukakamilika katika siku zijazo.

Ujumbe mwingine muhimu ni kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina azma thabiti na ya dhati ya kuwatetea washirika wake. Hizbullah ya Lebanon ni miongoni mwa washirika muhimu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambapo Tehran tayari ilitangaza uungaji mkono wake kwa Hizbullah ilipoanzisha vita dhidi ya Israel.

Ujumbe mwingine muhimu unahusiana na umoja wa medani ya vita katika mhimili wa upinzani. Kinyume na madai ya utawala wa Kizayuni, si tu kwamba mhimili wa muqawama katika eneo hili haujatoweka wala kudhoofika, bali umoja wa wahusika wa muqawama umedhihirika zaidi, kwa namna ambayo mara tu baada ya shambulio la makombora la Iran katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, Yemen pia ilivurumisha makombora dhidi ya Wazayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Kwa hiyo, umoja wa medani na mshikamano wa wanachama wa muqawama pia umeongezeka.

Ujumbe mwingine muhimu ni msimamo thabiti wa Iran katika kutetea umoja wa ardhi ya nchi za Kiarabu huku ulimwengu wa Kiarabu ukiwa umenyamaza kimya mbele ya uvamizi na ukaliaji mabavu wa utawala wa Kizayuni wa ardhi za Waarabu. Utawala wa Kizayuni umeikalia kwa mabavu sehemu ya jiografia ya nchi hizo kufuatia mashambulizi yake ya mara kwa mara katika eneo la kusini mwa Lebanon, ambapo inasikitisha kuona kwamba nchi za Kiarabu zimekaa kimya na kutoonyesha kuguswa na suala la utawala ghasibu wa Israel kuendelea kupora na kukalia kwa mabavu ardhi za nchi za Kiarabu. Utawala wa Kizayuni katika siku za nyuma ulikalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Syria, na nchi za Kiarabu kutoguswa wala kuchukua hatua yoyote ya kukabiliana na uvamizi huo. Hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa jibu la kijeshi kwa uchokozi na jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel unaoikalia kwa mabavu Lebanon. Ujumbe mwingine muhimu ni kwa Marekani. Kwa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya utawala wa Kizayuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefikisha ujumbe kwa Marekani kwamba haiko tayari kuzisaliti pande za muqawama katika meza ya mazungumzo na kwamba makubaliano yatafikiwa tu pale vita vitakapomalizika na kusimamishwa katika medani zote za vita. Kwa hatua hii ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, sasa mpira uko katika uwanja wa Marekani kuona ikiwa itafanikisha mapatano na Tehran au itaendelea kuyakwamisha kwa kutoa matakwa ya kupindukia na yasiyotekelezeka kimantiki.

Nukta ya mwisho ni kwamba, vita kati ya utawala wa Kizayuni na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ijapokuwa vimekuwa vya muda mfupi na kumalizika katika muda wa chini ya saa 24, lakini vimeonyesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitauruhusu utawala wa Kizayuni kuendelea kuvuruga mlingano wa nguvu katika eneo la Asia Magharibi kupitia vitendo vya uharibifu, vya kichokozi na haramu vinavyotekelezwa kwa uungaji mkono kamili wa Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *