Polisi wa Kenya wametumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya raia waliokuwa wakiandamana huko Nanyuki leo Jumanne kupinga kuanzishwa kituo cha karantini cha Marekani ndani ya kambi ya kijeshi ili kuwapokea raia wa Marekani wanaoshukiwa kuwa na Ebola.
Maandamano hayo – ambayo yaliandaliwa karibu na kituo cha anga cha Laikipia huko Nanyuki – yameshuhudia mapigano kati ya Polisi wa Kenya na waandamanaji waliokuwa wakipinga mradi huo.
Video zilizorushwa hewani na Al Jazeera Live zimeonyesha sehemu ya mapigano kati ya polisi na waandamanaji waliokuwa na hasira, ambayo yalisababisha moshi na moto karibu na eneo hilo, huku kukiwa na idadi kubwa na askari usalama.
Shirika la Habari la Ufaransa limeripoti kuwa, Polisi wa Kenya wamewakamata waandamanaji kadhaa huko Nanyuki na kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji.
Maandamano ya leo yanafuatia maandamano kama hayo mapema mwezi huu ambayo yalisababisha vifo vya watu wawili katika mji wa Nanyuki, baada ya polisi kuwafyatulia risasi mamia ya waandamanaji waliokuwa wamekusanyika karibu na kambi ya Laikipia.
Hasira ya umma ilizuka nchini Kenya kuhusu mpango wa kuanzisha kitengo cha kutengwa washukiwa wa Ebola chenye vitanda 50 ndani ya Kituo cha Anga cha Laikipia ili kuwapokea Wamarekani wanaoshukiwa kuwa wameambukizwa virusi hivyo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo au Uganda.
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu walifanya maandamano wiki iliyopita mjini Nairobi wakipinga makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya nchi hiyo na Marekani ya kuanzisha nchini Kenya kituo cha kuhifadhi Wamarekani wanaoshukiwa kuambukizwa virusi vya Ebola.
Mahakama Kuu ya Kenya ilitoa uamuzi wa kuongeza muda wa kusimamishwa mradi huo kwa wiki 3 zaidi, baada ya hapo awali kuusitisha kutokana na kesi iliyowasilishwa na shirika la kutetea haki za binadamu.
Jaji Patricia Nyaundi alitoa maagizo hayo Ijumaa baada ya kundi la kutetea haki kupinga mradi huo, likisema kuwa unazua masuala ya kikatiba na ya maslahi ya umma yanayohitaji mapitio ya kimahakama.
Licha ya uamuzi huo wa mahakama, vyanzo vya kidiplomasia na afisa mmoja wa Marekani viliripoti kwamba ndege za kijeshi za nchi hiyo ziliendelea kusafirisha wafanyakazi na vifaa hadi eneo hilo katika siku za hivi karibuni, ikionyesha kwamba maandalizi ya yalikuwa yakiendelea.
Kituo hicho kilichopendekezwa kimeibua mjadala mkali nchini Kenya, kufuatia taarifa kwamba kitatumika kuwashughulikia raia wa Marekani wanaoweza kuwa wameathiriwa na Ebola wakati wa mlipuko unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Vilevile kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kuwa Marekani haitawaruhusu kuingia nchini humo waathirika au washukiwa wa ugonjwa wa Ebola na kwamba watatibiwa katika nchi nyingine imewakasirisha sana Wakenya wanaoona kwamba nchi yao inatumiwa kama jaa la taka na Marekani.