s

Chanzo cha picha, Getty Images

Kombe la Dunia 2026 linaanza Juni 11, yamesalia saa chache tu. Mataifa yako katika hatua za mwisho mwisho, makocha wakikamilisha mipango yao, huku mashabiki wakisubiri kuanza kwa mashindano haya ya soka makubwa zaidi duniani.

Lakini kabla hata ya kipyenga cha kwanza kupulizwa, mjadala mwingine tayari umechukua nafasi kubwa mtandaoni, kuhusu jezi zitakazotumika na mataifa mbalimbali.

Kutoka Ulaya hadi Afrika, baadhi ya mataifa yamepongezwa kwa ubunifu wa hali ya juu, huku mengine yakikosolewa kwa kukosa mvuto na ubunifu unaotarajiwa kwenye mashindano makubwa kama Kombe la Dunia.

Jezi zilizowavutia mashabiki

s

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Kwa mujibu wa maoni ya mashabiki na wadau wa soka mitandaoni, jezi za ugenini za Uruguay, Japan na Ufaransa ni miongoni mwa zilizovutia zaidi kuelekea Kombe la Dunia 2026.

Muonekane wake, rangi zisizo za kawaida na simulizi zilizofichwa nyuma ya ubunifu wake zimezifanya zipate sifa nyingi kwenye majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii.

Jezi ya ugenini ya Uruguay ndiyo imekuwa gumzo zaidi na kubwa kutokana na muonekano wake wa kipekee unaokumbusha historia ya taifa hilo katika soka la dunia. Jezi hiyo ya rangi ya samawati iliyokolea imebuniwa kama kumbukumbu ya kikosi cha Uruguay kilichoshinda Kombe la Dunia la kwanza mwaka 1930.

Sehemu ya shingoni ina mapambo ya rangi ya bluu na machungwa yanayofanana na silaha za jadi za wenyeji wa Amerika Kusini, jambo linaloipa mwonekano wa kisasa huku ikihifadhi urithi wa kihistoria.

Jezi ya ugenini ya Japan, nayo imepokelewa vizuri kutokana na muundo wake uliovutwa kutoka kwenye jezi za zamani za mchezo wa baseball. Jezi hiyo yenye rangi ya krimu nyepesi imepambwa kwa mistari 12 myembamba ya upinde wa mvua, ambapo 11 inawakilisha wachezaji uwanjani na mstari mwekundu wa katikati ukiwakilisha familia nzima ya soka la Japan. Muonekano wake wa kipekee ulisababisha jezi hiyo kuuzwa kwa haraka mara baada ya kuzinduliwa.

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa upande wa Ufaransa, jezi yao ya ugenini imevutia wengi kutokana na rangi yake ya kijani iliyochochewa na sanamu maarufu ya Statue of Liberty nchini Marekani, ambayo ilitolewa zawadi na Ufaransa katika karne ya 19. Nembo za rangi ya shaba na mapambo ya rangi za bendera ya Ufaransa kwenye mikono ya jezi hiyo yameongeza mvuto wake. Wengi wameisifu kwa kuunganisha historia, utamaduni na ubunifu wa kisasa katika muundo mmoja unaovutia macho.

Barani Afrika, Nigeria imeendelea kuthibitisha sifa yake ya kuwa miongoni mwa mataifa yenye jezi zinazovutia zaidi duniani. Muundo wake umeonekana kuchanganya ubunifu wa kisasa na utambulisho wa Kiafrika kwa namna iliyowafurahisha wengi.

Jezi ya Morocco nayo imepongezwa kwa muundo wake safi, wa heshima na unaoakisi urithi wa taifa hilo la Afrika Kaskazini.

Jezi zilizozua ukosoaji mkubwa na kukosolewa

S

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Sio kila taifa limefanikiwa kuwashawishi mashabiki. Jezi za Uruguay, Ureno na Uholanzi zimeonekana kuwa nzuri na za kawaida, lakini kwa baadhi ya mashabiki zimekosa ubunifu wa kipekee.

Kwa wengi, ni jezi ambazo zinatajwa kama salama mno : hazina kosa kubwa, lakini pia haziachi kumbukumbu ya kudumu.

Pia baadhi ya mataifa yamejikuta yakikosolewa vikali mitandaoni kutokana na muonekano wa jezi zao.

Jezi ya Qatar imeelezewa na baadhi ya mashabiki kuwa ya kawaida mno na inayofanana na mavazi ya mazoezi.

Kwa Misri, mashabiki wengi walitarajia kuona mguso wa historia na utamaduni wa taifa hilo, lakini wengine wameeleza kusikitishwa na muundo waliouona kuwa wa kawaida.

China nayo imekosolewa kwa kukosa ubunifu, huku jezi ya Cameroon ikigawa maoni baadhi wakisifu matumizi ya rangi zake, wengine wakisema imepoteza mvuto wa kisasa.

Kwa wengi, Kombe la Dunia si mashindano ya kandanda pekee.

Ni tamasha la utamaduni, historia na utambulisho wa kitaifa. Na jezi zimeendelea kuwa sehemu muhimu ya namna mataifa yanavyojitambulisha mbele ya dunia.

Wakati mashabiki wakisubiri kuona nani atakayebeba kombe mwaka 2026, tayari mjadala wa jezi ipi nzuri na ya kuvutia kwenye Kombe la Dunia la mwaka 2026?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *