Chalamila atembelea kituo cha TFF KigamboniChalamila atembelea kituo cha TFF Kigamboni

DAR ES SALAAM: MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema ujenzi wa kituo Uwanja Cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Kigamboni uwekezaji mkubwa unaochochea maendeleo ya uchumi wa eneo husika pamoja na kuinua hadhi ya Kigamboni na Jiji la Dar es Salaam kwa ujumla.

Akizungumza leo Juni 10, wakati wa ziara yake katika kituo hicho, Chalamila amesema ameamua kutembelea mradi huo kwa sababu tatu kuu. Kwanza, kujionea matumizi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, akisisitiza kuwa kiongozi anatakiwa kushuhudia kwa macho maendeleo yanayotekelezwa badala ya kusikia taarifa pekee.

Pili, amesema kuthibitisha madai kwamba vituo vya maendeleo ya michezo vinachangia kuibua vipaji na kuboresha matokeo ya timu za taifa.

Ameeleza kuwa mafanikio yanayoonekana kwa sasa yanaonyesha kuwa uwekezaji katika miundombinu ya michezo una mchango mkubwa katika kukuza uwezo wa wachezaji.

Sababu ya tatu amesema ni kujifunza na kuona ni mambo gani Serikali inaweza kuyaiga kutoka katika mradi huo ili kuyaeneza katika maeneo mengine.

Amesema yupo katika nafasi ya kuunganisha Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, hivyo ni muhimu kujifunza mbinu bora zinazoweza kuhamishwa na kutekelezwa katika maeneo mengine.

Chalamila amesisitiza umuhimu wa kuwa na mpango endelevu wa kuendeleza vipaji vya michezo (succession plan), akieleza kuwa mafanikio ya sasa hayawezi kudumu bila kuwekeza kwa watoto, makocha, walimu na wadau wengine wa michezo.

Aidha, amesema mafanikio katika michezo hayawezi kutegemea sababu moja pekee kama kocha au mchezaji mmoja, bali yanatokana na ushirikiano wa wadau wengi wakiwemo makocha, wachezaji, viongozi, wazazi na jamii kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa ameipongeza TFF kwa kuwekeza katika kituo hicho cha kisasa, huku akiitaka mamlaka ya TARURA kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa barabara zinazoelekea katika eneo hilo ili kuendana na thamani ya uwekezaji uliofanyika.

Pia amesisitiza umuhimu wa kujenga mifereji ya maji sambamba na barabara, akibainisha kuwa maji ndiyo adui mkubwa wa miundombinu ya barabara, hasa katika maeneo ya Kigamboni ambayo hupokea maji mengi wakati wa mvua.

“Tukijenga barabara bila mifereji ya maji, tutakuwa tunajenga miundombinu ambayo itaharibika kwa haraka. Lazima tuhakikishe mifereji inajengwa ili kulinda uwekezaji wetu,” amesema Chalamila.

Kwa Upande wake, Colnel Barnabas, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania amesema kituo hicho kimegharimu zaidi ya Sh bilioni 4 na kina mchango mkubwa na kina manufaa kwa wachezaji hivyo kinatumika na kina tija.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *