
Baada ya mtanange wa ghuba ya Ua Jeni kukaza, si Tarampu akajifyatua ufahamu na kuanzisha vita ya lapdogs na Fyatuland! japo Tarampu ni fyatu uchwara, si aliwafyatua lapdogs wangu eti wasiende majuu kujienjoi!
Nilipata habari hii mbaya nikiwa pipani nikielekea majuu kwa Put in. Nisharejea wanoko msianze kutafuta mambo yangu na kunifyatua. Sikujua kuwa Tarampu anafyatuka vibaya.
Si aliamua kuwafyatua lapdogs eti kwa vile walirarua wanakondoo! Alisema wasikanyage Umarekanini! Nilishangaa sana.
Kwani, wanakondoo wangu wanamhusu nini yarabi? Kutaka sifa na kukimbia kipigo cha maajemi si Tarampu akajifyatua na kuwafyatua bila kujali kuwa wanafanya kazi zangu! Ukijifyatua na kunichokoza au kutaka kunifyatua, nawaamuru wakufyatue haraka sana.
Kwa vile mie ni Fyatu zaidi ya Tarampu, nilimwonya. Kama ataendelea na ufyatu wake uchwara, nitazuia wake kuingia Fyatuland. Akiendelea nampiga marufuku hata yeye kuingia Fyatuland. Mambo ya Fyatuland yanamhusu nini au anadhani mie ni kama Maduro aje animaduro? Athubutu aone kilichofanya ngamia kuwa na nundu. Shauri yake.
Nimegundua kuwa Tarampu ni mwoga wa kaiwada na bingwa wa mikwara uchwara. Huenda anatingisha kibiriti kwa kutumia vita ya lapdogs ili anifyatue au anaogopa kunifyatua. Vinginevyo anataka kunitia kashkash ili apata namna ya kuifyatua Fyatuland kama alivyoifanyia Venezuela.
Maana, haiinigi akilini ang’ang’anie kufyatua lapdogs ilhali mwenyewe nipo. Najiuliza bila majibu. Inakuwaje?
Huwezi kung’atwa na chawa ukawalaumu zaidi ya yule aliyewafuga au kuacha kuwateketeza. Mnaninyaka hapa? Imenishangaza sana. Eti dogii kuwararua wanakondoo anaadhibiwa bila kujali nani alimwamuru awararue!
Kwani kazi ya dogii ni nini kama siyo kuwafyatua wengine kwa amri ya mwenye kumfuga? Nadhani amewaonea wivu lapdogs wangu niliowalisha wakanenepeana wakati wake wanakondeana.
Kama siyo hivyo, basi uzee unamuijia vibaya. Haiingii akilini. Unamuadhibuje mbwa na siyo mwenye mbwa? Kweli, hii ni haki? Wahenga waliasa kuwa ukimuona dogii, jua kuna mwenyewe.
Na dogii hafanyi kitu bila amri ya mwenye kumfuga. Inakuwaje unamwadhibu mbwa na kumuacha amfugaye? Kwanini kumfyatua mjumbe wakati aliyetuma humfyatui? Sasa natangaza vita.
Natangaza vita ya wanene na siyo guard dogs wao. Kama ataendelea kubwekabweka, nitamfanyia kitu ambacho hajawahi kufanyiwa Fyatu yoyote. Huwezi kuwaandama lapdogs wangu nami nikakuacha. Hapa, Tarampu ajue. Tutafyatuana hadi kieleweke.
Inaonekana wadukuzi wake ni wavivu wa kufikiri na kudukua. Kama hajui ni kwanini wanakondoo walifyatuliwa na attack dogs wangu si aniulize nimpe inshu nzima badala ya kutishiana kufyatuana na asifyatuke na kufyatua.
Kwa nini Tarampu hataki kukubali kuwa wanakondoo walivyatuliwa kwa sababu walitaka kujigeuza mbwa mwitu halafu wanifyatue? Kwanza, namjuza Tarampu na wengine wanaojifyatua ufahamu. Wajue na wakome na kukomaa. Lapdogs wangu si washari. Ukiona wamewafyatua wanakondoo, ujue kuna kitu wanakondoo walitaka kufyanya.
Maana, haiingii akilini kuwaacha wanakondoo waliozoea kuishi kwa amani kujigeuza mbwa mwitu. Ili iweje kama siyo kunifyatua mie mwenye kuwatunza?
Pili, namuonya Tarampu na wenzake wanaodhani wanaweza kunifyatua. Najua. Wameanza na lapdogs wangu ili baadaye nifuate. Sitakubali.
Tarampu, who are you? Kama wana kondoo wangekuwa wake, lau angekuwa na hoja. Mambo ya Fyatu amuachia Fyatu mwenyewe. Hayamhusu hata kidogo.
Tatu, hakuna kondoo walioraruriwa toka Fyatuland.
Waliofyatuliwa ni wa kaya ya jirani waliofyatuka na kutaka kuwafundisha umbwa mwitu kondoo wangu waaminifu na wasio na hatia wala washari.
Nne, namuonya kwa mara ya mwisho Tarampu. Asitake kutuletea ubeberu na kujitia ufahari asijue nasi tunauweza huo ubeberu wake. Tarampu ajue.
Mie simshobokei wala kumnyenyekea eti kwa vile ana njuluku. Si alikata misaada kwa Fyatuland baada ya kukataa ubeberu uchwara wake. Kuna Fyatu amekufa kwa kukatiwa hiyo misaada yake?
Tano, Tarampu ajue hanitishi. Na kama ni ufyatu mie ndo mfalme wa Mafyatu akiwamo yeye. Lazima tuheshimiane. Aniheshimu. Aheshimu dog wangu.
Akiendelea kujifyatuafyatua, nitamuwekea vikwazo vya kiuchumi. Angejua kuwa kupeleka lapdogs wangu kwenye kaya yake kulikuwa kunamuingizia njuluku kibao, asingejifyatua na kutaka eti kuwafyatua dog wangu wapendwa.
Sita, kama Tarampu ataendelea na ubeberu wake, nitaanza kufanya mipango ya kutengeneza bomu la nyukilia ili kiumane. Anadhani siwezi? Akamuulize Kiduku ambaye amekuwa akimtoa jasho. Hapa, sijagusia kwenda kwa swahiba yangu Xii Jin Pingu ampige pingu. Nlishaonya. Fyatuland inawenyewe na wenyewe ni sisi. Hatutishwi wala kuyumbishwa.
Tunatesa kwa raha zetu. Hata kama nitaamuru attack dogs wawafyatue wanakondoo tena, yeye inamhusu nini. Si akafyatue wake waligeuka mbwa mwitu zamani kiasi cha kufyatuana wao kwa wao kwa vile dog wake hawana uwezo wa kuwafyatua.
Mwisho, ni vizuri Tarampu akajuzwa na kujua. Du! Kwani, nimesemaje? Naongelea lapdog au madogii? Kumbe naota nikipata kichapo cha dirisha la Horumuziiii Uajemiii!