Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kwamba idadi ya visa vilivyothibitishwa vya Ebola imepanda na kukaribia 600, huku kukiendelezwa uhamasishaji miongoni mwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua za kujikinga.

Mripuko wa aina ya Bundibugyo ya Ebola ulitangazwa tarehe 15 Mei, ingawa maafisa wameeleza tangu wakati huo kwamba ugonjwa huo ulikuwa umeenea kwa majuma kadhaa bila kubainika, hali iliyoziacha mamlaka za afya zikiwa nyuma katika juhudi za kuudhibiti.

Moja ya milipuko mikubwa zaidi ya Ebola kuwahi kushuhudiwa duniani sasa inaendelea katika majimbo matatu yenye utajiri wa madini na ambayo kwa muda mrefu yamekumbwa na migogoro ya makundi yenye silaha: Ituri, Kivu Kaskazini, na Kivu Kusini.

Katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye X, serikali ya Congo imesema kufikia Jumanne idadi ya visa vilivyothibitishwa vya Ebola imeongezeka hadi 598, huku watu 115 wakiwa wamefariki hadi sasa

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa wagonjwa 22 wamepona ugonjwa huo, na kwamba visa vipya havijasambaa hadi maeneo mengine zaidi ya afya.

Visa hivyo vimerekodiwa katika maeneo 17 ya afya ya Ituri, pamoja na maeneo saba ya afya katika Kivu Kaskazini na eneo moja la afya katika Kivu Kusini.

Taarifa hiyo ilisema, huku ikiwahimiza wananchi kufuata maelekezo ya wahudumu wa afya na kutowashambulia. Aidha wananchi wameshauriwa kuwa iwapo wana dalili za homa, kutapika, kuharisha, au udhaifu mkubwa, wanapaswa kwenda mara moja kwenye kituo cha afya kilicho karibu kupata matibabu.

Kutokuaminiana na upinzani kutoka kwa baadhi ya wananchi kumeathiri juhudi za kukabiliana na mlipuko huo, huku mashambulizi dhidi ya timu za maziko na vituo vya matibabu yakiripotiwa.

Kwa mujibu wa madaktari zaidi ya dazeni moja, wahudumu wa misaada ya kibinadamu na maafisa wa afya ya umma, watabibu pia wanakabiliwa na ugumu wa kupata vifaa vya msingi vya kujikinga na kuzuia kusambaa zaidi kwa ugonjwa huo.

Shirika la misaada la International Rescue Committee Jumanne lilitoa wito wa kutolewa kwa ufadhili unaohitajika ili kuudhibiti mripuko huo katika jimbo la Ituri kabla haujasambaa zaidi.

Aidha, Idara ya Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) imeonya kwamba juhudi zinazoendelea za kukabiliana na Ebola “zinakabiliwa na vikwazo vikubwa vya kiutendaji.”

Taarifa hiyo imesema kuwa vituo vya afya katika maeneo kadhaa yaliyoathiriwa viko katika hali mbaya na mara nyingi havina maji salama ya kunywa, vichomea taka, vifaa vya kujikinga binafsi, pamoja na vifaa vya kuondoa vimelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *