
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, ametangaza mpango huo mjini Geneva, Uswisi, nakueleza kuwa ni jibu la moja kwa moja kwa hali ya dunia ambayo ameitaja kuwa “iko katika sintofahamu kubwa.”
Akizungumza na idhaa ya Umoja wa Mataifa Kamishna Türk amesema muungano huo umeundwa ili kuunganisha nguvu na ari ya watu wanaotaka kuona mabadiliko chanya duniani.
Dunia Bora Zaidi
“Watu wengi duniani wanataka dunia bora zaidi, wanataka dunia yenye usawa zaidi na haki zaidi,” amesema Kamishna Türk nakuongeza kuwa“Haki za binadamu ni sehemu ya utu wao. Ni sehemu ya maumbile yetu.”
Muungano huo unalenga kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo serikali, asasi za kiraia, wafanyabiashara, miji, viongozi wa dini, wasanii, wasomi na vijana chini ya mfumo wa pamoja unaojengwa juu ya misingi mitatu: kufikiri, kujadiliana, na kuchukua hatua .
Waraka wa dhana uliochapishwa na OHCHR unaeleza kuwa mfumo wa haki za binadamu duniani unakabiliwa na “shinikizo ambalo halijawahi kushuhudiwa,” huku ukiukwaji wa haki za binadamu ukiendelea bila wahusika kuwajibishwa, nafasi za kiraia zikizidi kupungua, baadhi ya mataifa yakijiondoa katika ahadi za ushirikiano wa kimataifa, na ukosefu mkubwa wa fedha ukitishia mfumo mzima wa haki za binadamu.
Hatua za vitendo
Mwezi huu, Muungano huo utaanza kutekeleza mipango kadhaa ya vitendo ikiwemo:
- Kituo cha Kimataifa cha msaada kuhusu biashara na haki za binadamu
- Mkutano wa RightsX Summit kuhusu ubunifu wa kidijitali;
- Programu ya “Haki za binadamu katika kila darasa” inayolenga kujumuisha elimu ya haki za binadamu katika ngazi zote za elimu.
Aidha, Türk ametangaza lengo la kuongeza mtandao wa Miji ya Haki za Binadamu kutoka miji 104 iliyopo sasa hadi miji 1,000 duniani kote.
Kuwapa waathirika sauti
Akizungumzia suala la fidia na uwajibikaji, Türk amesisitiza umuhimu wa kusikiliza waathirika wa ukiukwaji wa haki za binadamu.
“Moja ya mambo muhimu zaidi ni kuwapa sauti waathirika wa ukiukwaji wa haki za binadamu na waathirika wa migogoro.”
Ametaja raia walioathiriwa na vita na migogoro huko Ukraine, Gaza, Lebanon, Myanmar, Sudan na Haiti kama mifano ya watu wanaohitaji kusikilizwa na kupata haki.
Wajibu wa wenye nguvu
Mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa pia amezungumzia nguvu inayozidi kushikiliwa na makampuni makubwa ya teknolojia, akionya kuwa haki za binadamu zinapaswa kuwa mwongozo na mfumo wa udhibiti wakati ambapo nguvu kubwa za kifedha na kisiasa zinatumika.
Mpango wa muda mrefu
Muungano huu umeundwa kuwa juhudi za muda mrefu badala ya kampeni ya muda mfupi, ukiwa na hatua muhimu ya miaka mitatu kuelekea maadhimisho ya miaka 80 ya Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu (UDHR) yatakayofanyika tarehe 10 Desemba 2028.
Jukwaa la Mwaka la Muungano wa Kimataifa wa Haki za Binadamu litafanyika kila mwaka katika tarehe hiyo ili kutathmini maendeleo yaliyopatikana na kuweka vipaumbele vya hatua zinazofuata.
KamishnaTürk amesema Geneva imechaguliwa kuwa nyumbani kwa mpango huo kutokana na uwepo wa taasisi nyingi za haki za binadamu, lakini akasisitiza kuwa, “Muungano huu utakuwa na makao kila mahali, popote ambapo haki za binadamu zinajadiliwa.”