Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Ulaya, Hans Henri P. Kluge, amesema hakuna wagonjwa wa Ebola katika nchi zinazoshiriki kuandaa mashindano hayo wala katika eneo la Ulaya. “Hakuna sababu ya kubadili mipango yenu. Safirini kama kawaida, endeleeni kupata taarifa sahihi na furahieni mashindano hayo”.

WHO yasisitiza umakini licha ya hatari kuwa ndogo

Dkt. Kluge amewataka wasafiri kuwa makini na dalili za Ebola, ikiwemo homa, maumivu ya mwili na kutapika, hasa kwa wale waliotembelea hivi karibuni maeneo yaliyoathiriwa nchini Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo DRC au Uganda. “Ikiwa umesafiri hivi karibuni kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Uganda na ukajihisi mgonjwa ndani ya wiki tatu baada ya kurejea, tafuta huduma za afya mara moja na umweleze daktari wako historia ya safari yako,” amesisitiza. 

Ameongeza kuwa ukaguzi wa kawaida wa afya mipakani na katika matukio makubwa ni hatua muhimu za kulinda afya ya umma.

Mafanikio ya kudhibiti wagonjwa yadhihirisha uwezo wa mfumo wa afya

WHO imeeleza kuwa mgonjwa mmoja wa Ebola aliyesafirishwa kutoka Uganda kwa matibabu kwenda nchini Ujerumani alipona baada ya kuwekwa katika uangalizi maalum wa kutengwa. Watu watano waliokuwa wamekaribiana naye walifuatiliwa kwa siku 21 bila yeyote kuugua. “Kwa sasa hakuna wagonjwa wa Ebola katika Kanda ya Ulaya, na muhimu zaidi hakuna maambukizi ya ndani. Hatari ya jumla inaendelea kuwa ndogo,” amesema Dkt. Kluge, akisisitiza kuwa mifumo ya ufuatiliaji na maandalizi ya afya imeimarika.

Sababu zinazofanya hatari kubaki chini

Kwa mujibu wa WHO, wagonjwa wengi wa Ebola kwa sasa wameripotiwa katika maeneo ya mbali ya DRC, huku hatua za uchunguzi wa afya zikitekelezwa kabla ya safari kutoka maeneo yaliyoathirika. 

Shirika hilo limefafanua kuwa Ebola haisambai kwa njia ya hewa, bali kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa na ambaye tayari anaonesha dalili za ugonjwa huo

Ingawa bado hakuna chanjo iliyoidhinishwa au tiba maalum kwa aina hii ya Ebola, WHO inasema huduma za mapema za matibabu zinaweza kuokoa maisha na mifumo ya afya katika Kanda ya Ulaya iko tayari kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza.

WHO yatoa wito wa huruma na mshikamano wa kimataifa

Dkt. Kluge pia ameonya dhidi ya unyanyapaa kwa watu kutoka maeneo yaliyoathiriwa na Ebola pamoja na jamii za Waafrika. 

“Kuenea kwa Ebola hakuamuliwi na utaifa au kabila la mtu,” amesema. “Unyanyapaa huwafanya watu waogope kutafuta huduma za afya na unaweza kufanya milipuko ya magonjwa kuwa vigumu zaidi kudhibitiwa.” 

Amesisitiza kuwa njia bora ya kulinda watu duniani kote ni kukomesha mlipuko huo katika chanzo chake, akibainisha kuwa WHO na washirika wake wanaendelea kuunga mkono juhudi za kukabiliana na Ebola DRC na Uganda. 

“Kwa kutumia tahadhari, taarifa sahihi na huruma kwa wengine, tunaweza kuwalinda watu na kuhakikisha mchezo unaendelea salama,” amehitimisha.

Soka kwa malengo ya dunia

Na wakati dunia ikielekeza macho yake kwenye Kombe la Dunia la FIFA 2026, Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa kwa Ulaya Magharibi (UNRIC) kinaangalia mashindano hayo kupitia mtazamo wa Ulaya na Umoja wa Mataifa, kikisisitiza masuala ya wakimbizi, ujumuishaji wa jamii, afya, usawa na hatua za vitendo ambazo mashabiki wanaweza kuchukua ili kuunga mkono Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs)

Kwa mujibu wa UNRIC mashindano ya mwaka huu ndiyo makubwa zaidi kuwahi kufanyika, yakishirikisha 

  • Timu 48, zikiwemo timu 16 kutoka Ulaya. 
  • Aidha, wachezaji 11 wanaounda Timu ya Gamechanging ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) wana historia ya kukumbwa na kulazimika kuyahama makazi yao kutokana na migogoro na mateso. 
  • Takwimu za UNHCR zinaonesha kuwa watu milioni 117 duniani kote kwa sasa wamelazimika kuyakimbia makazi yao, jambo linaloonesha jinsi michezo kama soka inaweza kuwa jukwaa la kuhamasisha mshikamano, matumaini na mabadiliko chanya katika jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *