Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Tanzania inaendelea kuwekeza mabilioni ya fedha katika ujenzi wa barabara na madaraja ili kuboresha miundombinu na kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
Akizungumza na wananchi wa Kibada, Kigamboni, wakati ziara yake Wilaya ya Kigamboni kwenya Barabara ya Shangwe Kibada, Chalamila amesema Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 97 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Jangwani ambalo kwa miaka mingi limekuwa likikumbwa na changamoto za mafuriko na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara.
Amesema pamoja na mradi huo, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya madaraja mengine ikiwemo Mkwajuni na Nguvu Kazi ambapo fedha za mabilioni ya shilingi zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wake ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za usafiri kwa uhakika katika misimu yote ya mwaka.
Chalamila ameeleza kuwa katika Wilaya ya Kigamboni pekee, Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara inayounganisha maeneo ya makazi, biashara na uzalishaji, huku baadhi ya wakandarasi wakisimamia ujenzi wa zaidi ya kilometa 10 za barabara kwa wakati mmoja.
Mkuu huyo wa Mkoa alitumia fursa hiyo kueleza kuwa maendeleo yanayoshuhudiwa nchini yanatokana na mchanganyiko wa mapato ya ndani kupitia kodi pamoja na fedha zinazopatikana kupitia ushirikiano wa maendeleo na taasisi mbalimbali za kifedha.
“Ni kweli miradi mingi inajengwa kwa fedha za kodi za Watanzania, lakini kodi pekee hazitoshi kugharamia mahitaji yote ya maendeleo. Serikali inalazimika pia kutafuta fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati,” alisema Chalamila.
Aliwataka wananchi kutambua mchango wa Serikali katika kusaka vyanzo mbalimbali vya fedha vinavyowezesha utekelezaji wa miradi ya barabara, madaraja, shule, hospitali, huduma za maji na umeme katika maeneo mbalimbali ya nchi.
(Feed generated with FetchRSS)