MTWARA: MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli Nchini (PURA) imesema hadi sasa tanzania imeshagundua kiasi cha gesi asilia futi za ujazo trilioni 57.54 katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mnazi Bay kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.

Hayo yamebainishwa wakati Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka hiyo na kamati zake ilipotembelea miradi ya gesi asilia kwenye halmashauri hiyo kwa lengo la kujifunza na kujionea utendaji kazi wake.

Miradi hiyo ikiwemo eneo la uchimbaji wa kisima cha utafutaji wa gesi asilia cha kasa kilichopo Mnazi Bay pamoja na kiwanda cha kuchakata gesi asilia iliyozalishwa Mnazi Bay cha Madimba na kwa sasa kiasi kikubwa cha umeme takribani asilimia 35 ya umeme unaotumika Tanzania unatokana na gesi asilia.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni amesema maeneo mbalimbali yaliyogunduliwa gesi hiyo asilia yamekuwa yakifanyiwa mwendelezo ili kuitoa kule ambako imegunduliwa kuja juu ya ardhi na kufanyiwa matumizi.

“Sasa tukaona ni vema tukaongeza idadi ya visima ili tuongeze kiasi cha uzalishaji cha gesi ambayo nyingi inaenda kwenye mitambo ya madimba ambayo inamilikiwa na TPDC na ndiyo gesi inayotumika kufulia umeme,”amesema Sangweni

Naye, Mwenyekiti wa Bodi, Halfani Halfani amesema ziara hiyo imewasaidia kujua uchimbaji au uzalishaji wa gasi asili namna ambayo unafanyika.

Pia amezungumzia namna  watanzania kwa ujumla wanavyonufaika na rasirimalia hiyo ikiwemo wanamtwara hasa uwepo wa mzungunguko mkubwa wa fedha zinazoletwa na miradi hiyo katika jamii kama vile barabara na mingine.

Kwa upande wake Mhandisi Mwandamizi wa Petroli PURA, Fabian Mwose amezungumzia hatua ya awali ya utafutaji wa gesi kwenye kisima cha kasa kuwa ni cha tatu katika kampeni ya visima vitatu vya gesi asilia ambacho kimeanza kutobolewa Juni 1, 2026.

Uchimbaji huo unatarajiwa kutumia siku hamsini na tano baada ya hapo kutafanyika maandalizi ya kisima kwa ajili ya uzalishaji pale ambapo watakuwa wamegundua uwepo wa gesi asilia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *