Akizungumza mjini Geneva Uswisi hii leo, Mwakilishi wa UN Women nchini Haiti, Marie Goretti Nduwayo, amesema kuwa nyumba hizo salama, zinazojulikana kama Women’s Houses, ni hatua muhimu katika kukabiliana na ongezeko la ukatili wa kijinsia.

“Ufunguzi wa makazi haya ni wakati wa matumaini, lakini pia ni ukumbusho wa maumivu na hatari zinazowakabili wanawake na wasichana nchini Haiti,” amesema.

Magenge yatumia ubakaji kama silaha ya kutisha jamii

Bi. Nduwayo amesema taarifa kutoka kwa wanawake na wasichana zinaonesha kuwa ubakaji unatumika kwa kiwango kikubwa na magenge kama njia ya kutisha, kudhibiti na kuadhibu jamii.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa mwaka 2025 kulithibitishwa visa 1,863 vya ukatili wa kingono, ikiwemo wanawake 1,668 na wasichana 187, ongezeko la asilimia 163 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu pekee, zaidi ya asilimia 70 ya visa vyote vya ukatili wa kijinsia vilivyoripotiwa vilihusisha ukatili wa kingono. “Ubakaji unazidi kutumiwa kama silaha ya ugaidi na udhibiti wa jamii. Tunaona hilo wazi katika simulizi za wanawake na katika takwimu,” ameonya.

Wakimbizi wa ndani wako katika hatari kubwa zaidi

Kuenea kwa ghasia za magenge kutoka mji mkuu Port-au-Prince hadi maeneo mengine ya nchi kumewalazimu karibu watu milioni 1.47 kuhama makazi yao, wakiwemo wanawake na wasichana 790,000.

Kwa mujibu wa UN Women, maeneo yote 22 ya wakimbizi wa ndani yaliyofanyiwa tathmini yaliripoti matukio ya ukatili wa kijinsia. Ukosefu wa taa, vyoo visivyo salama na kutokuwepo kwa huduma tofauti kwa wanawake na wanaume kunachochea hatari zaidi.

“Wanawake wanaoishi katika maeneo ya wakimbizi wanakabiliwa na baadhi ya viwango vya juu zaidi vya hatari ya ukatili,” amesema Bi. Nduwayo.

Maumivu ya kisaikolojia na kuporomoka kwa huduma za msingi

UN Women imesema athari za kisaikolojia za ghasia hizo ni kubwa sana. Wanawake wengi wameeleza kuwa hawawezi tena kutambua maisha yao ya zamani baada ya kushuhudia nyumba zikichomwa moto, wapendwa wao kuuawa na kulazimika kukimbia huku wakifuatwa na watu wenye silaha.

Wakati huo huo, zaidi ya shule 1,600 zimefungwa na karibu asilimia 40 ya vituo vya afya katika mji mkuu Port-au-Prince havifanyi kazi tena.

“Wanawake huniambia kuwa ukatili walioupitia unaendelea kuwafuata mchana na usiku, hata wanapolala,” amesema Bi. Nduwayo.

Licha ya mateso, wanawake waongoza juhudi za msaada

UN Women imesema pamoja na changamoto hizo, wanawake wa Haiti wameendelea kuwa mstari wa mbele katika juhudi za kibinadamu, amani na usalama.

Ushiriki wao katika kamati za kusimamia maeneo ya wakimbizi umeongezeka kutoka asilimia mbili mwaka 2024 hadi zaidi ya asilimia 40 mwaka 2025. Mashirika ya wanawake yanasaidia manusura wa ukatili, kutoa misaada ya fedha taslimu, kusaidia familia kupata huduma muhimu na kuimarisha ulinzi wa jamii. “Wanawake wa Haiti si waathirika tu, pia ni viongozi wanaosaidia jamii zao kuhimili na kujikwamua kutokana na mgogoro huu,” amesisitiza mwakilishi huyo wa UN Women.

Wito wa msaada wa haraka wa kimataifa

UN Women imeonya kuwa mahitaji yanaendelea kuongezeka wakati misaada ya kimataifa kwa Haiti ikipungua kwa kiwango kikubwa.

Shirika hilo limetoa wito wa kuongezwa kwa huduma za kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia, msaada wa chakula na fedha taslimu, huduma za afya na elimu, pamoja na uwekezaji zaidi katika mashirika yanayoongozwa na wanawake. “Wanawake na wasichana wa Haiti wameonesha mnepo wa ajabu, lakini mnepo pekee hauwezi kuwa jibu,” amesema Bi. Nduwayo. “Wanahitaji usalama, ulinzi na hatua za haraka kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *