Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva  Uswisi baada ya kutembelea Bunia, kitovu cha mlipuko huo, Dkt. Douglas Noble wa UNICEF amesema mazingira ya migogoro ya muda mrefu, utapiamlo na huduma dhaifu za afya yanawaweka watoto katika hatari kubwa zaidi.

“Tayari watoto hawa wako katika mazingira magumu sana. Uwezo wa jamii kuhimili mshtuko wowote wa ziada ulikuwa umefikia ukomo kabla hata Ebola haijafika,” amesema.

© UNICEF/Josue Mulala Msaada wa dharura unatayarishwa kupelekwa katika jimbo la Kasaï kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Ebola uliotangazwa hivi karibuni nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hofu yachangia watoto kukosa huduma muhimu

Dkt. Noble amesema wahudumu wa afya katika Hospitali ya Rwampara wamemweleza kuwa watu wengi wameacha kwenda hospitalini kwa huduma za kawaida kwa hofu ya kuambukizwa Ebola.

Ameonya kuwa hali hiyo inaweza kusababisha madhara makubwa kwa watoto. “Familia zinapoacha kutafuta huduma za afya, watoto hukosa chanjo na magonjwa mengine hayapatiwi matibabu. Hapo mlipuko unaanza kuua maisha ambayo haukuyaathiri moja kwa moja,” amesema.

Maambukizi ya kifamilia yanaweza kuongeza watoto waathirika

Kufikia tarehe 11 Juni, DRC ilikuwa imeripoti wagonjwa 676 waliothibitishwa wa Ebola na vifo 136.

Ingawa wengi wa walioambukizwa hadi sasa ni watu wazima wenye shughuli za kijamii na kiuchumi, UNICEF inaonya kuwa maambukizi yanapoenea ndani ya familia watoto wanaweza kuathirika zaidi.

“Kadri mlipuko unavyoendelea, lazima tujiandae kuona maambukizi zaidi ndani ya kaya, jambo linalomaanisha kuwa tunaweza kuona watoto wengi zaidi wakiathirika katika siku zijazo,” amesema Dkt. Noble, akibainisha kuwa dalili za Ebola kwa watoto mara nyingi hufanana na malaria, hali inayochelewesha utambuzi wa ugonjwa huo.

Uelewa mdogo wa jamii wazua wasiwasi

UNICEF pia imeeleza wasiwasi kuhusu kiwango cha chini cha uelewa wa jamii kuhusu Ebola.

Kwa mujibu wa utafiti wa U-Report uliowahusisha vijana 50,000 nchini DRC, theluthi mbili hawakujua jinsi ugonjwa huo unavyoenea wala namna ya kujikinga, huku mmoja kati ya watano akisema haamini kuwa Ebola ni ugonjwa halisi. “Imani na uelewa wa jamii haviwezi kuchukuliwa kuwa vitu vya kawaida. Kujenga uaminifu kati ya wataalamu wa afya na jamii ni muhimu ili kudhibiti mlipuko huu,” amesisitiza.

© WHO/Joël Lumbala Vifaa vya msaada vya kukabiliana na mlipuko wa Ebola nchini DR Congo vinawasilishwa kwa helikopta UN .

UNICEF yaongeza msaada huku ikiomba ufadhili zaidi

UNICEF imesema tayari imepeleka tani 150 za vifaa vya dharura Bunia, kuwafundisha na kupeleka zaidi ya wahudumu na wanahamasishaji wa afya 1,600, pamoja na timu 24 za usafishaji ambazo zimefikia kaya zaidi ya 160,000. Shirika hilo pia linafungua vituo salama vya kulelea watoto karibu na vituo vya matibabu ya Ebola.

Hata hivyo, Dkt. Noble amesema mafanikio yatategemea upatikanaji wa rasilimali, ufikishaji wa misaada na ushirikiano wa jamii.

“DRC na Uganda zimewahi kudhibiti Ebola hapo awali, na kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa zinaweza kufanya hivyo tena,” amesema, huku UNICEF ikiomba dola milioni 70.7 kwa miezi sita ijayo ili kuendeleza mapambano dhidi ya mlipuko huo.

Wagonjwa wapya wanabainika kila siku: WHO

“Kila siku, wagonjwa wanatambuliwa katika maeneo mapya ya afya. Hilo linaonesha kwa kweli ukubwa wa mlipuko huu, ambao ni mkubwa zaidi kuliko idadi ya wagonjwa wanaogunduliwa, pamoja na kiwango kikubwa cha watu kuhama-hama katika sehemu hii ya DRC,” amesema Dkt. Olivier le Polain, mkuu wa kitengo cha epidemiolojia na uchambuzi wa hatua katika Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO).

Katika kipindi cha takriban wiki tatu tangu mlipuko huu unaosambaa kwa kasi uthibitishwe, mamlaka za afya za DRC zimeripoti wagonjwa 676 wa Ebola na vifo 136 vilivyosababishwa na aina adimu na hatari ya virusi vya Ebola vya Bundibugyo.

Maambukizi yamegunduliwa katika eneo linaloanzia Aru kaskazini mwa jimbo la Ituri hadi Miti Murhesa katika jimbo la Kivu Kusini, umbali wa takriban kilomita 1,000. “Kufikia jana tulikuwa na maeneo 34 ya afya yaliyoathiriwa, na maeneo hayo yanaendelea kuongezeka huku maeneo mapya ya Kivu Kaskazini pia yakiripoti wagonjwa jana,” Dkt. le Polain amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kupitia mawasiliano ya video kutoka Beni.

Wanaoongoza juhudi za kukabiliana na mlipuko huo wamesisitiza kuwa watoto wengi katika eneo hilo wanakabiliwa na utapiamlo na hawajapata chanjo dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika. Hali hiyo inawafanya kuwa katika hatari kubwa ya kuugua katika eneo lenye utajiri wa rasilimali lakini ambalo tayari linakabiliwa na mzozo wa kibinadamu uliosababishwa na miongo kadhaa ya mapigano kati ya vikosi vya serikali na makundi yenye silaha.

© UNICEF/Mark Naftalin Afisawa UNICEF akizungumza na msichana akiosha mikono yake katika hatua ya kuzuia kusambaa kwa ugonjw wa Ebola ,Kivu Kaskazini ,DRC.

Shule zinaweza kuendelea kuwa wazi

Ingawa Ebola inaweza kuwa ugonjwa hatari unaoua, husambaa kwa njia tofauti kabisa na coronavirus“>COVID-19, na mara nyingi kupitia majimaji ya mwili. Kwa sababu hiyo, watoto wanaoweza kwenda shule wanapaswa kuendelea kufanya hivyo, afisa wa UNICEF amesisitiza.

“Hakuna sababu ya shule kufungwa. Hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi lazima zichukuliwe, na elimu kuhusu ugonjwa huo itolewe shuleni kwa walimu, wafanyakazi na watoto wenyewe.”

Tofauti na aina ya Ebola-Zaire, kwa sasa hakuna dawa maalumu zilizoidhinishwa wala chanjo maalumu dhidi ya virusi vya Bundibugyo. Hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuongeza msaada kwa shughuli za ufuatiliaji wa maambukizi ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo, amesema Dkt. le Polain.

“Kwa sasa tumefikia zaidi ya asilimia 70 ya watu waliokutana na wagonjwa ambao wanafuatiliwa ipasavyo. Hayo ni maendeleo makubwa ukilinganisha na hali ilivyokuwa wiki moja au mbili zilizopita, lakini bado kiwango hicho ni cha chini mno kuhakikisha udhibiti wa kutosha wa mlipuko.”

Kuimarisha uwezo wa upimaji wa maabara katika maeneo husika pia ni jambo muhimu katika kukabiliana na tishio hili la kiafya, kwani ukubwa kamili wa mlipuko huo “bado haujafahamika kikamilifu”, ameeleza afisa huyo wa WHO.

Amebainisha kuwa maabara ya Beni ilichakata vipimo 500 katika siku moja tu ya Alhamisi. “Hilo litatusaidia sana kupata picha sahihi ya ukubwa wa mlipuko huko Beni pia,” ameongeza.

Kwa upande wake, UNICEF  imeongeza kuwa “Tunaweza kuwaepusha watoto na madhara makubwa zaidi ya mlipuko huu. Ugunduzi wa haraka wa wagonjwa, huduma bora za afya kwa watoto, ufuatiliaji wa watu waliokutana na wagonjwa pamoja na jamii zilizoelimishwa na kushirikishwa zinaweza kusaidia kuudhibiti mlipuko huu,” amesema Dkt. Noble.

Ameongeza kuwa “Ambacho tunahitaji sasa ni rasilimali za kutosha, upatikanaji wa misaada ya kibinadamu na ushirikiano wa jamii ili kufanikisha juhudi hizi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *