Utafiti huo, ulioongozwa na watafiti kutoka HRP,  Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO na Chuo Kikuu cha Oxford, unakadiria kuwa wanawake milioni 27 huathiriwa na PPH kila mwaka, huku takribani wanawake 43,000 wakifariki dunia kutokana na tatizo hilo. Aidha, hali hiyo hugharimu zaidi ya dola bilioni 10 za Marekani kila mwaka.

Akizungumza kuhusu matokeo hayo, Profesa Arri Coomarasamy wa Chuo Kikuu cha Oxford amesema “Kutokwa na damu baada ya kujifungua kunaweza kuwapata wanawake wote. Tunahitaji kuboresha namna tunavyokabiliana na tatizo hili ili kuokoa maisha zaidi.”

Wagonjwa wengi hawagunduliki mapema

Watafiti wamebaini kuwa makadirio ya macho ya kiasi cha damu kinachopotea mara nyingi hayatoi matokeo sahihi, jambo linalosababisha wagonjwa wengi kutogunduliwa mapema.

Ripoti hiyo inapendekeza matumizi ya vifaa vya kupima damu inayopotea na kuanza matibabu mapema kwa wanawake wanaoonesha dalili za hatari.

Pia inapendekeza matumizi ya kifurushi cha huduma za dharura kinachojulikana kama MOTIVE, ambacho kinaweza kupunguza kwa hadi asilimia 60 hatari ya hali hiyo kuwa ya kutishia maisha.

Wataalamu pia wanasisitiza umuhimu wa kuzuia upungufu wa damu wakati wa ujauzito, kuboresha huduma za uzazi wa mpango na kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kusaidia mfuko wa uzazi kujikaza baada ya kujifungua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *