Zaidi ya shilingi milioni 300 zimetumika kujenga jengo la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, vyoo pamoja na mnara wa maji katika Kituo cha Afya Namwawala kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba. Mradi huo unatarajiwa kuboresha huduma za afya kwa wananchi zaidi ya 10,000 wa eneo hilo na maeneo ya jirani.
Akizungumza na Channel Ten baada ya Mwenge wa Uhuru kutembelea na kukagua mradi huo, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Namwawala, Maria Joseph, amesema kukamilika kwa miundombinu hiyo kutapunguza kwa kiasi kikubwa adha ya wananchi waliokuwa wakisafiri zaidi ya kilometa 40 kufuata huduma za matibabu katika maeneo mengine.
Akimkaribisha Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Dustan Kyobya amesema kabla ya mradi huo wananchi walilazimika kutembea umbali mrefu kupata huduma za afya, hali iliyokuwa ikiwasababishia usumbufu mkubwa na gharama za ziada.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, amesema ameridhishwa na ubora wa utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa utaleta manufaa makubwa kwa wananchi kwa kusogeza huduma muhimu za afya karibu zaidi na makazi yao.
Baadhi ya wananchi wa eneo hilo, akiwemo Charles Matonya na Hidaya Mohamed, wamepongeza kukamilika kwa mradi huo wakisema utarahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu na kupunguza gharama za usafiri walizokuwa wakitumia kutafuta huduma hizo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Dkt. Rose Rwakatare, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuimarisha huduma za afya na kuboresha ustawi wa wananchi kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
(Feed generated with FetchRSS)