Taarifa inafafanua zaidi kwamba, miongoni mwa vijana balehe, wasichana walichangia zaidi ya asilimia 61 ya wagonjwa hao, yaani wagonjwa 27 kati ya 37 waliothibitishwa kwa vipimo vya maabara.

UN Women inaeleza ikisema, “uhalisia wa mlipuko huu wa sasa unafuata mwelekeo ule ule ambao historia imekuwa ikituonesha mara kwa mara: wanawake na wasichana huathirika zaidi katika milipuko ya Ebola. Maambukizi ya ugonjwa huu hufuata hali halisi za kijamii, yakisambaa kupitia majukumu ya ulezi, kazi za nyumbani, huduma za afya mstari wa mbele na taratibu za mazishi zinazowaweka wanawake na wasichana katika mawasiliano ya karibu na wagonjwa wakati wa hatua za maambukizi ya ugonjwa.”

Hali hii ilishuhudiwa pia katika mlipuko wa Ebola wa mwaka 2018–2019 nchini DRC, ambapo wanawake na wasichana walichangia takriban theluthi mbili ya visa vilivyoripotiwa. Hata mwaka 1976 nchini humo, wanawake walikuwa asilimia 56 ya watu wote waliofariki kutokana na ugonjwa huo.

Zingatia: Takwimu za sasa ni kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO, kufikia tarehe 7 Juni 2026.

Ili kubadili mwelekeo huu, “tunahitaji uwekezaji mkubwa zaidi katika programu za huduma za msingi za afya zinazozingatia mahitaji halisi ya wanawake na wasichana. Hii inamaanisha kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kujikinga binafsi (PPE) na vifaa vya kinga dhidi ya maambukizi, pamoja na kuwekeza katika mafunzo na uongozi wa wanawake katika shughuli za jamii za uhamasishaji na kinga dhidi ya Ebola.” Inasema UN Women na kuongeza kuwa hatua hizi ni muhimu kwa utambuzi wa mapema wa ugonjwa na utoaji wa huduma salama.

Pia ni muhimu kuwekeza katika uthabiti na kwa njia inayobadilika kulingana na mahitaji katika mashirika yanayoongozwa na wanawake. Mashirika hayo tayari yako mstari wa mbele na yana jukumu muhimu katika mawasiliano ya wakati wa dharura, yakihakikisha taarifa sahihi na zinazookoa maisha zinawafikia wanawake na jamii zao, huku yakizuia kuenea kwa taarifa potofu. “Ufadhili endelevu ndio unaowezesha kazi hii kuendelea na kupanuka,” inasisitiza taarifa ya UN Women.

UN Women, inafanya kazi moja kwa moja katika nchi zilizoathiriwa na Ebola kwa kushirikiana na serikali, mfumo wa Umoja wa Mataifa na mashirika yanayoongozwa na wanawake. Jukumu lake ni kuunga mkono na kuimarisha juhudi zao, huku likihakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika kufanya maamuzi kuhusu kinga, mwitikio na hatua za kupona baada ya mlipuko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *