
TIMU ya JKT Tanzania imeshindwa kutamba nyumbani katika mechi ya Ligi Kuu baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam ikiwa ni ushindi wa kulipiza kisasi.
Katika mechi hiyo, Singida ilitangulia kupata bao lililofungwa na Mkongomani Horso Mwaku dakika ya 23 baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa JKT Tanzania na kutumia vyema pasi ya kiungo nyota wa kikosi hicho, Emmanuel Keyekeh.
Wakati JKT Tanzania ikitengeneza mashambulizi kwa ajili ya kusawazisha, ilichapwa bao la pili lililofungwa na Emmanuel Keyekeh dakika ya 75, baada ya kupiga shuti la kushtukiza nje ya eneo la 18, lililomshinda kipa, Ramadhan Chalamanda.
Hata hivyo, jitihada za JKT zilizaa matunda dakika ya 81, baada ya kufunga bao la kufutia machozi lililofungwa na nyota wa kikosi hicho, Valentino Mashaka aliyemaliza mpira uliopigwa na Hassan Kapalata na kupigwa kichwa kilichoingia wavuni.
Ushindi huo kwa Singida ni wa kisasi, kwani mechi ya raundi ya kwanza kati ya timu hizo iliyopigwa Januari 20, 2026, ikiwa uwanja wa nyumbani, ilichapwa bao 1-0, lililofungwa na kiungo mshambuliaji wa JKT, Salehe Karabaka dakika ya 81.
Kichapo hicho kinaifanya JKT kufikisha mechi nne mfululizo za Ligi Kuu bila ya ushindi, huku mara ya mwisho kwa kikosi hicho kushinda ilikuwa ni Mei 9, 2026, ilipoifunga Mbeya City bao 1-0, kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni.
Matokeo hayo yanaifanya Singida kubakia nafasi ya nne na pointi 44, baada ya kushinda 13, sare tano na kuchapwa minane, huku JKT ikishika nafasi ya sita na pointi 38, ikishinda tisa, sare 11 na kupoteza sita, kufuatia zote kucheza mechi 26.