Mbeya. Usiku ambao wengi walikuwa wamelala kwa utulivu, kwa Catherine Fatika (80) na wajukuu wake ulikuwa mwanzo wa simulizi ya maumivu, hofu na mapambano ya kila siku ya kuendelea kuishi.
Imeelezwa siku ya tukio mvua kubwa ilinyesha ikiambatana na upepo mkali Februari mwaka huu na kuibomoa nyumba waliyokuwa wakiishi katika Mtaa wa Tonya, Kata ya Ilomba jijini Mbeya, huku wote wakiwa ndani wamelala.
Kutokana na kadhia hiyo, ni miezi kadhaa sasa familia hiyo imekuwa ikiishi katika kibanda cha pembeni kisicho salama, huku hofu ya kubomokewa tena ikitawala maisha yao kila siku.
Leo, Jumamosi Juni 13, 2026, baada ya miezi ya mateso na maisha duni, tabasamu linaanza kurejea baada ya Taasisi ya Tulia Trust kuanza rasmi ujenzi wa nyumba mpya kwa ajili ya familia hiyo.
Mbali na kupoteza makazi, Catherine amedai kupata majeraha yaliyosababisha ulemavu wa miguu na mkono wa kushoto, hali iliyomfanya ashindwe kujihudumia na kutegemea wajukuu wake kwa karibu kila jambo.
“Tulilazimika kuishi kwenye nyumba hii ya pembeni ambayo nayo si salama. Kila siku tunaishi kwa hofu kwamba inaweza kubomoka wakati wowote,” amesema Catherine.
Bibi Catherine Fatika (80) akiwa na wajukuu zake pamoja na mmoja wa majirani zake muda mfupi baada ya nyumba aliyokuwa akiishi kubomolewa kupisha ujenzi wa makazi mapya ya kisasa unaotekelezwa na Taasisi ya Tulia Trust, leo Jumamosi, Juni 13, 2026. Picha na Hawa Mathias.
Amesema maisha yake yamekuwa ya mateso kutokana na kushindwa kutembea na kutegemea msaada wa watu wengine hata kwa mahitaji ya msingi.
“Nahitaji mtu wa kunitoa nje kuota jua, kunirudisha ndani na kunisaidia kwenda chooni. Wajukuu wangu wakiwa shuleni nabaki peke yangu bila msaada,” amesema kwa sauti ya huzuni.
Mbali na makazi mapya, Catherine anatamani pia kupata msaada wa matibabu na chakula ili kurejesha afya yake na kuwapunguzia mzigo wajukuu wake.
“Hapa naishi na wajukuu zangu watatu, lakini mama yao ambaye ni mkwe wangu aliolewa na mwanangu ambaye ni marehemu. Yuko kutafuta riziki, akipata anakuja kuleta kwa ajili ya mahitaji mbalimbali, lakini shida ni kwamba sina uwezo wa kunyanyuka pasipo msaada,” amesema.
Mjukuu wake, Callshma Mathias (16), mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Sekondari Ilomba, amesema familia yao imekuwa ikipambana na changamoto nyingi huku wakijitahidi kuendelea na masomo.
“Mama yetu hana kazi ya kudumu. Akipata vibarua ndipo tunapata chakula na mahitaji mengine. Sisi tunapokuwa shuleni, bibi hubaki peke yake ndani kwa sababu hakuna wa kumhudumia,” amesema.
Amesema siku za mwisho wa wiki ndizo wanazopata nafasi ya kumtoa bibi yao nje, kumpeleka chooni na kumsaidia shughuli nyingine za kila siku.
“Bibi yetu anaumwa. Tunaomba msaada wa matibabu na mahitaji mengine, ikiwemo chakula, ili tuweze kumudu mahitaji mbalimbali ya hapa nyumbani,” amesema.
Akizungumza wakati wa kuanza ujenzi wa nyumba hiyo, Mwakilishi wa Taasisi ya Tulia Trust, Kitengo cha Mawasiliano, Hady Kalinjila, amesema taasisi hiyo iliguswa na hali ya familia hiyo baada ya kubaini mazingira hatarishi waliyokuwa wakiishi.
“Tumebaini kuwa wanaishi katika mazingira magumu na yasiyo salama. Kwa kuanzia, tumeanza ujenzi wa makazi bora ili kurejesha heshima na matumaini yao ya maisha,”amesema.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Taasisi ya Tulia Trust za kuwafikia wananchi wenye mahitaji maalumu na kurejesha tabasamu katika jamii.
Pia ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na kutokuwa kikwazo katika utekelezaji wa mradi huo ili familia hiyo ipate makazi salama kwa wakati.
Kwa upande wake, mkazi wa Mtaa wa Tonya, Joyce Daimon, amesema ujenzi wa nyumba mpya utamaliza hofu ambayo familia hiyo imekuwa ikiishi nayo tangu nyumba yao ilipobomoka.
“Tunashukuru kwa msaada huu. Ombi letu ni kwamba pamoja na kujengewa nyumba, kikongwe huyu apatiwe pia matibabu ili aweze kurejea katika hali nzuri ya afya,” amesema.