
Dar es Salaam. Kadiri idadi ya magari inavyoongezeka katika Jiji la Dar es Salaam, ndivyo umuhimu wa kuwa na mfumo bora wa usimamizi wa maegesho unavyozidi kuonekana.
Serikali na mamlaka za mitaa zimekuwa zikitegemea ukusanyaji wa ada za maegesho kama chanzo cha mapato na njia ya kudhibiti matumizi ya maeneo ya umma.
Hata hivyo, pamoja na nia hiyo nzuri, baadhi ya watumiaji wa magari wanasema utekelezaji wa mfumo huo bado una changamoto zinazohitaji kufanyiwa maboresho.
Changamoto kubwa inayolalamikiwa katika Mkoa wa Dar es Salaam na baadhi ya madereva ni kuhusu namna magari yanavyoskaniwa (scan) na kuandikiwa ada za maegesho katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Wapo wananchi wanaodai mfumo uliopo hauzingatii mazingira halisi ya matumizi ya gari, hali inayosababisha baadhi yao kujikuta wakitozwa ada mara kadhaa ndani ya muda mfupi au hata kuongezewa madeni yasiyo halali.
Wananchi waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti wamesema ili mfumo wa ada za maegesho ukubalike zaidi kwa wananchi, ni muhimu kuwepo kwa uwazi, urahisi wa kufuatilia taarifa za malipo na matumizi ya teknolojia itakayotambua tofauti kati ya gari lililoegeshwa na lile lililosimama kwa muda mfupi kutokana na shughuli za kawaida za usafiri wa mjini.
Malalamiko ya wananchi
Mei mwaka huu, kulishuhudiwa picha mjongeo iliyosambaa katika mitandao ya kijamii, ikimwonyesha mwananchi akimlalamikia mmoja wa maofisa wa usimamizi wa maegesho aliyekuwa akiscan magari yaliyokuwa kwenye msongamano wa barabarani.
Mwananchi huyo alisema magari yaliyokwama kwenye foleni hayapaswi kutafsiriwa kama yameegeshwa na kutozwa ada za maegesho.
Malalamiko kama hayo yalitolewa na mwananchi mwingine aliyedai kuwa baadhi ya watoa huduma wamekuwa wakiscan magari hata yale yaliyoegeshwa katika makazi ya watu.
Kilio hichohicho kilitolewa na Joseph Elias, mkazi wa Dar es Salaam, aliyesema kumekosekana utaratibu maalumu wa kusimamia shughuli ya kuscan magari, jambo linalosababisha gari moja kuskaniwa mara kadhaa ndani ya muda mfupi.
Amesema dereva anaweza kuegesha gari katika mtaa mmoja na likatozwa, kisha akihamia eneo jingine ndani ya muda huohuo akakutana na wahudumu wengine wanaofanya kazi hiyo na kuandikiwa tena ada ya maegesho.
“Sasa huwa najiuliza mifumo haisomani hadi hali hii inatokea? Kwa sababu usipofuatilia kiwango cha deni unalodaiwa, unaweza kujikuta una malimbikizo makubwa ya ada za maegesho,” amesema Elias.
Kwa mujibu wake, changamoto nyingine ni wahudumu wa maegesho kuscan gari mara tu linaposimama bila kutoa muda wa kutosha kwa dereva kuendelea na safari au kuamua kama ataegesha kwa muda mrefu.
“Hii si sawa. Wakati mwingine mtu anasimamisha au anageuza tu gari, lakini anajikuta amepigwa picha kwa ajili ya kulipa ada ya maegesho,” amesema Elias.
Mkazi mwingine wa Dar es Salaam, Enock Goodluck, amesema mfumo huo umekuwa mzigo kwa baadhi ya watumiaji wa magari kutokana na ada na faini zinazoongezeka haraka.
“Unaweza kuegesha gari kwa dakika chache ukaandikiwa ada, halafu ukitoka kwenda eneo jingine ukaandikiwa tena. Kwa shughuli zangu za hapa mjini, wakati mwingine deni la maegesho linaweza kufikia Sh10,000 nisipoilipa kwa wakati kutokana na faini,” amesema.
Goodluck amesema wakati mwingine mfumo huonyesha madeni ya maeneo aliyowahi kuegesha siku kadhaa zilizopita licha ya kutorudi tena katika maeneo hayo.
“Unaweza kuegesha gari Ubungo Plaza, kwa mfano Mei 15, lakini Mei 17 ukiangalia mfumo unakuta bado kuna deni la eneo hilo ilhali hukurudi tena hapo. Hii imekuwa changamoto kubwa kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri jijini Dar es Salaam,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, ameshauri kuwepo kwa muda maalumu kabla gari halijaandikiwa ada ya maegesho ili kutoa nafasi ya kutofautisha kati ya gari lililoegeshwa na lile lililosimama kwa muda mfupi.
Aidha, amesema ni muhimu kuanzishwa kwa maeneo rasmi ya maegesho ya muda mrefu yatakayowezesha madereva kuyaacha magari yao na kuendelea na shughuli nyingine bila hofu ya kuongezewa ada mara kwa mara.
Mbali na hilo, ameshauri Serikali kuboresha mfumo wa kukusanya madeni ya maegesho kwa kutumia teknolojia na mifumo rafiki zaidi badala ya kutegemea hatua za utekelezaji zinazohusisha vyombo vya dola.
Dereva aliyewahi kukamatwa eneo la Gongo la Mboto, Amin Msomali, amesema alikuta ana deni la Sh5,000 na alipouliza maeneo aliyoegesha alionyeshwa barabara ambayo amekuwa akipita na si kusimama.
“Niliandikiwa sehemu tofauti. Kuna moja niliambiwa nimeegesha Sinza, sehemu ambayo sijawahi kusimama zaidi ya kupita. Nikaambiwa niliegesha dukani kwa Vunja Bei, mahali ambapo sijawahi hata kwa bahati mbaya kusimamisha gari,” amesema.
Walichokisema mameya
Akizungumza na Mwananchi kuhusu suala hilo, Meya wa Kinondoni, Songoro Mnyonge, amesema wameshawasilisha changamoto hiyo Tamisemi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) kwa sababu mfumo wa kulipa ada za maegesho unasimamiwa na ofisi hiyo.
Mnyonge amedai kosa lililopo katika mfumo huo ni kutoeleza muda halisi ambao gari lililoegeshwa limekaa.
“Hatua hii inampa nafasi ofisa aliyeruhusiwa kuchanja magari kukutoza hata mara 10. Hili ndilo ambalo linaleta maneno mengi, maana hata mimi ninavyoomba vya usafiri, kuna wakati nashangaa gari inadaiwa Sh9,000 au Sh10,000 hadi unajiuliza ilikwenda wapi wakati ipo ndani tu.
“Hii ni changamoto, ndiyo maana Kinondoni tumewaambia Tamisemi wakae waangalie hili jambo. Zamani mtu akikuchanja anakuwekea stakabadhi kwenye kioo cha gari, inakuwa rahisi kujua umekaa muda gani. Kama saa mbili, atakuwekea stakabadhi mbili,” ameeleza Mnyonge.
Mbali na hilo, Mnyonge amesema Dar es Salaam ipo tofauti na mikoa mingine, akieleza ukitembea kidogo unajikuta umeingia Manispaa ya Ilala au Manispaa ya Ubungo kutokana na ukaribu wa manispaa hizo, hivyo kuna umuhimu wa mifumo hiyo kusomana.
“Kwa sababu manispaa zote tunaingiliana, ile saa moja iwe ya kuegesha Dar es Salaam, si kwa halmashauri moja pekee. Nikienda Ilala, wakichanja igome ionyeshe nimeshaskaniwa wilaya nyingine na saa moja haijaisha. Ndiyo maana tumepeleka haya mapendekezo Tamisemi, tunasubiri majibu,” amesema Mnyonge.
Meya wa Manispaa ya Temeke, Uzairu Athuman, amesema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto hiyo ambayo inapaswa kufanyiwa kazi.
Athuman amesema kwa upande wao wataishauri Tamisemi kuboresha mifumo hiyo ili iweze kusomana na kufanya kazi kwa ufanisi.
“Lengo la Serikali ni kuwa na mifumo rafiki itakayomwezesha mwananchi kuchangia kupitia maegesho rasmi kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi, na si kumnyonya mwananchi,” amesema.
Wanaochanja wafunguka
Baadhi ya watumishi wanaofanya kazi ya kuchanja magari yanayoegesha mkoani Dar es Salaam, kwa masharti ya kutotaja majina yao, wamesema chanzo kikuu cha hali hiyo ni shinikizo la kufikia malengo wanayopewa na waajiri wao.
“Mfanyakazi yeyote huwekewa malengo ya kazi, hivyo nalazimika kufanya kila linalowezekana kuyafikia ili kulinda ajira yangu ya kibarua,” anaeleza mtoa huduma huyo.
Amesema kila siku asubuhi wanapopangiwa mitaa ya kufanyia kazi hupewa kiwango cha mapato wanachotakiwa kukusanya. Kwa mfano, katika maeneo yenye msongamano wa magari kama Kariakoo, malengo huanzia Sh200,000 na kuendelea kwa siku.
“Ukifanya kazi kwa ufanisi, kila mwisho wa mwezi unapewa kamisheni. Hilo ndilo linalowachochea watumishi wengi kujituma na kuwa katika maeneo yao muda wote,” amesema.
Amekiri wamekuwa wakipokea na kusikia malalamiko ya wananchi kuhusu mfumo wa maegesho, lakini akasema suala hilo linapaswa kushughulikiwa na mamlaka husika, ikiwemo Tamisemi.
“Kuna nyakati wananchi wenye hasira hutufuata na kulalamika kuwa wamewekewa madeni makubwa ilhali hawakuegesha katika maeneo ya maegesho. Sisi huwa tunawaeleza kuwa maeneo hayo ni mali ya Serikali, hivyo tunaruhusiwa kuchanja magari popote ndani ya mtaa tuliopangiwa kufanya kazi,” amesema.
Mwingine anayefanya shughuli hiyo amesema wanakumbana na changamoto nyingi wakati wa kutekeleza majukumu yao, hususan kutokana na uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi wanaoamini wamebambikiwa madeni.
“Kwa mfano, kama nimepangiwa Mtaa A, jukumu langu ni kuhakikisha magari yote yaliyoegeshwa katika eneo hilo yanalipia ada ya maegesho ya Sh500 kwa saa. Kila baada ya saa moja nachanja upya.
“Gari likihamia mtaa mwingine, mtumishi aliyepo huko naye analichanja ili kufikia malengo aliyowekewa,” amesema.
Amesema changamoto nyingine ni baadhi ya watumishi wa umma, hususan wanaoendesha magari yao binafsi na kuyaegesha katika maeneo hayo, lakini hawataki magari yao kuchanjwa.
“Wakati mwingine hutokea mvutano na hatimaye tunalazimika kuwaacha, jambo ambalo hutuumiza kwa sababu magari hayo huendelea kuegeshwa kwa muda mrefu bila kulipia.
“Pia, baadhi ya watumishi hutumia magari ya Serikali na kuyaegesha kwa muda mrefu katika maeneo hayo, hali ambayo huwa changamoto kubwa kwetu kwa sababu hatuwezi kuyascan,” amesema.
Serikali kufuatilia
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Festo Dugange ameahidi kulifuatilia suala hilo ili kujua undani wa changamoto zinazolalamikiwa na wananchi kuhusu ada za maegesho.
“Nafahamu kuna utaratibu wa maegesho unaopaswa kulipiwa ndani ya muda fulani ukiwa ndani ya halmashauri moja. Kama upo nje ya halmashauri, labda ulikuwa Kinondoni ukaenda Ubungo au Ilala ndani ya muda mfupi, hapo kutakuwa na suala ambalo inabidi tulifuatilie.
“Sina uhakika changamoto hiyo inatokana na nini. Nafuatilia nijue tatizo ni nini hadi wananchi wanalalamika na kupata taarifa za kutosha ili niweze kutolea maelezo,” amesema Dk Dugange.