
Shirika la Afya Duniani (WHO) jana Ijumaa lilitangaza kuwa mlipuko wa Ebola kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo sasa unaenea katika maeneo mapya.
WHO imesema kuwa hatua zaidi zinahitajika ili kudhibiti msambao wa virusi vya Ebola.
Tangu kutangazwa mlipuko wa ugonjwa huo Mei 15 mwaka huu kumethibitishwa kesi 676, ikiwa ni pamoja na vifo 136 vilivyothibitishwa huko Kongo.
Watu 119 wanashukiwa kuwa na maambukizi ya Ebola huku wagonjwa 32 wakipona kabisa ugonjwa huo.
Hadi sasa hakuna chanjo au tiba kwa ajili ya spishi adimu ya Bundibugyo inayotajwa kusababisha mlipuko wa sasawa ugonjwa wa Ebola, ambao umeathiri pakubwa mkoa wa Ituri, huku kesi nyngine zikigunduliwa katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Olivier Le Polain, mkuu wa WHO anayehusika na magonjwa na matibabu yake anasema: Mlipuko wa Ebola unaendelea kupanuka kwa upande wa idadi ya watu wanaoambukizwa lakini pia unazidi kuenea kwa upande wa maeneo ya kijiografia.
Akizungumza kutoka Beni katika jimbo la Kivu Kaskazini, Olivier Polain amesema kesi za maambukizi zinatambuliwa karibu kila siku katika maeneo mapya ya afya ndani ya majimbo matatu yaliyoathiriwa na ugonjwa huo. “Hali hii inadhihirisha wazi ukubwa wa mlipuko huu.”
Afisa huyo wa WHO amesema kuwa kiwango kamili cha mlipuko bado hakijawekwa wazi na kwamba wanataraji kupata ufafanuzi zaidi kadiri uchunguzi unavyoboreka.