
Mshambuliaji wa Brazil, Vinicius Junior, amelalamikia hali ya mazingira katika mashindano yanayoendelea ya Kombe la Dunia 2026.
Malalamiko hayo yamekuja baada ya timu ya taifa ya Brazil kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Morocco katika mchezo wao wa kwanza wa Kundi C uliochezwa jana Jumamosi, Juni 13, 2026.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Vinicius anayechezea klabu ya Real Madrid amesema kuwa Brazil ilipata ugumu wa kucheza kutokana na joto kali.
Ameeleza kuwa hali hiyo pia imeathiri mfumo wao wa mchezo na mbinu walizopanga kwa vile nyasi zilikuwa kavu.
“Joto ni kubwa muda wote, nyasi hukauka haraka sana, na mchezo unakuwa wa polepole mno.
“Tunashindwa kupata mdundo wetu wa kawaida, jambo ambalo linatuletea ugumu kwa sababu tunataka kucheza, tunataka kuhamisha mpira kutoka upande mmoja wa uwanja kwenda upande mwingine, na hali hii inaathiri mtindo wetu wa uchezaji,” amesema Vinicius Jr.
Brazil ilionekana kupata shida kudhibiti mchezo huo, na licha ya kutengeneza nafasi nyingi zaidi kipindi cha pili, ilishindwa kupata bao la ushindi.
Matokeo hayo yameifanya ipoteze pointi muhimu, jambo ambalo linaweza kuathiri nafasi zake za kumaliza kileleni mwa kundi.
Ismael Saibari aliifungia Morocco bao la kuongoza katika dakika ya 21 ya mchezo huo.
Hata hivyo, Brazil ilisawazisha kupitia kwa Vinicius Junior katika dakika ya 32 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Bruno Guimarães.
Baada ya mchezo dhidi ya Morocco, Brazil itakuwa na kibarua cha kuweka mambo sawa kwa kupata ushindi, itakapocheza dhidi ya Haiti katika mechi yake ya pili ya Kundi C itakayofanyika Jumapili, Juni 20.
Mchezo huo utachezwa katika uwanja wa Lincoln Financial Field uliopo Philadelphia.