
Dar es Salaam. Zaidi ya makontena 50 kwa siki yanatarajiwa kuanza kusafirishwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Dodoma kwa kutumia Reli ya Kisasa (SGR) kuanzia Julai 1, 2026, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa malori jijini Dar es Salaam na kuongeza ufanisi wa uondoshaji wa mizigo bandarini.
Foleni za malori katikati mwa Jiji la Dar es Salaam zimeendelea kuwa kero kwa watumia wa barabara hasa ya Mandela kutokana na uwepo wa wingi wa bandari kavu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, amesema kuanza kwa huduma hiyo kutasaidia kupunguza utegemezi wa usafirishaji wa mizigo kwa malori huku ikiongeza kasi ya uondoshaji wa mizigo bandarini.
Mbossa ametoa kauli hiyo leo Jumapili Juni 14, 2026 wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilipotembelea Bandari ya Dar es Salaam kukagua shughuli mbalimbali na maendeleo ya uwekezaji unaoendelea katika bandari hiyo.
Amesema kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam inapokea na kuhudumia kati ya makontena 100,000 hadi 150,000 kwa mwezi, kiwango ambacho kimekuwa kikisababisha ongezeko la malori yanayobeba mizigo kutoka bandarini kwenda maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
“Kuanzia Julai 1 tutaanza rasmi kusafirisha makontena kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Dodoma kwa kutumia reli ya SGR. Treni hii itasafirisha zaidi ya makontena 50 kwa siku. Kwa sasa bandari inahudumia kati ya makontena 100,000 hadi 150,000 kwa mwezi na kwa mji wa Dar es Salaam si rahisi kuhimili makontena yote haya, jambo ambalo linasababisha msongamano wa malori,” amesema Mbossa.
Mbali na hilo, amesema TPA ipo katika hatua za mwisho za kuhakikisha reli ya zamani ya MGR inaunganishwa kikamilifu na mfumo wa SGR ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini kwenda maeneo mbalimbali nchini na katika nchi jirani.
“Tunaendelea na hatua za mwisho kuhakikisha reli ya MGR inapokea mzigo unaoletwa na SGR. Hili litaongeza urahisi wa bandari yetu kufikika kwa haraka zaidi na kuongeza ushindani wake katika kuhudumia soko la kikanda,” amesema.
Amesema maboresho ya miundombinu na mifumo ya uendeshaji bandarini yanaendelea kufanyika ili kuendana na ongezeko la mizigo na mahitaji ya soko la kikanda, huku ushirikiano kati ya TPA, Shirika la Reli Tanzania (TRC) na wadau wengine ukiendelea kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya miradi hiyo.
Mbossa amesema mapato yanayokusanywa na bandari kwa sasa yana uwezo wa kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, huku TPA ikiendelea kushirikiana na sekta binafsi na taasisi za kifedha katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Devota Minja, amesema kamati hiyo imeridhishwa na maendeleo ya uwekezaji yanayoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha uwekezaji uliofanywa katika reli ya SGR na miundombinu ya bandari unaleta matokeo yaliyokusudiwa.
Amesema uwekezaji huo unapaswa kuongeza biashara, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha mapato ya Serikali kupitia ongezeko la mizigo inayopitishwa bandarini.
Awali, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema Bunge limekuwa na mchango mkubwa katika mageuzi yanayoendelea kwenye sekta ya bandari na kwamba matokeo ya uwekezaji huo sasa yanaonekana wazi kupitia ongezeko la mizigo inayohudumiwa.
“Wabunge mlisimama imara wakati wa kufanya maamuzi haya. Leo hoja imebadilika na kuwa namna ya kukabiliana na foleni ya mizigo kutokana na ongezeko kubwa la biashara. Waulizeni madereva wa malori wanavyopata kazi, waulizeni waendeshaji wa bandari kavu jinsi shughuli zilivyoongezeka. Tunajivunia msimamo huo ambao umeanza kuzaa matunda,” amesema Kihenzile.
Amesema ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari si jambo jipya duniani, bali ni mkakati unaotumiwa na bandari nyingi zinazofanya vizuri kimataifa ili kuongeza ufanisi wa huduma.
Kihenzile amesema kiwango cha mizigo inayosafirishwa kwenda nje ya nchi kimeongezeka kutoka tani milioni 5.6 hadi tani milioni 12.6, huku idadi ya makasha ikiongezeka kutoka 728,000 hadi zaidi ya milioni 1.08.
“Matokeo haya yanaonyesha mafanikio ya uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Tutaendelea kuimarisha sekta ya bandari kwa kujenga nyingine na kukamilisha miradi fungamanishi ikiwamo reli ya SGR,” amesema.
Kuanzishwa kwa usafirishaji wa makontena kwa kutumia SGR kunatarajiwa kuimarisha mnyororo wa ugavi wa mizigo nchini, kupunguza muda wa usafirishaji kutoka bandarini na kuongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia shehena kubwa zaidi kwa ufanisi, huku ikiendelea kuwa lango muhimu la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini.