
Bwana Yesu asifiwe wapendwa katika Kristo! Ninaitwa Mchungaji Gasper Madumla. Karibu kwenye tafakari ya Neno la Mungu leo Jumapili.
Ni neema kubwa kukutana katika kipindi hiki cha kujifunza Neno la Mungu. Ninaamini kwa rehema za Bwana mnaendelea vizuri pamoja na familia zenu na kwamba Mungu anaendelea kuwatendea makuu katika maisha yenu. Leo tutatafakari somo muhimu linalohusu upendo wa kweli, maana katika dunia ya leo watu wengi huzungumza kuhusu upendo lakini siyo wote wanaoufahamu au kuishi ndani yake.
Mungu atusaidie kupitia Neno lake ili tujue sifa za upendo wa kweli na namna ya kuutambua katika maisha yetu ya kila siku.
Neno la Msingi linatuongoza kwenye somo la leo linatoka(1 Wakorintho 13:4);
“Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni.”
Kuna tabia na sifa fulani unapoziona kwa mtu anayesema anakupenda unaweza kujua moja kwa moja kama anakupenda kwa dhati au anaigiza. Vivyo hivyo, mpenzi wako, ndugu yako au rafiki yako anaweza kutambua kama kweli unampenda au la.
Upendo wa kweli hauwezi kufichika kwa sababu huonekana katika matendo na mwenendo wa mtu.
Biblia inatufundisha sifa nyingi za upendo wa kweli, lakini leo tutajifunza sifa kuu tatu zinazotajwa katika 1 Wakorintho 13:4.
1. Upendo huvumilia
Uvumilivu ni uwezo wa kustahimili changamoto, maumivu, makosa ya watu au kuchelewa kwa mambo bila kukata tamaa, kulalamika au kuacha kufanya yaliyo mema.
Ni hali ya kuwa na subira na kuendelea kusimama katika imani hata katikati ya majaribu na mateso (Warumi 5:3-4; Yakobo 1:3-4; Waebrania 10:36).
Mungu mwenyewe ni mfano mkubwa wa uvumilivu. Kwa sababu anatupenda, huvumilia udhaifu wetu na huwapa watu nafasi ya kutubu na kubadilika.
Mifano ya Kibiblia
Bwana huvumilia kwa sababu hapendi mtu yeyote apotee (2 Petro 3:9; Warumi 2:4; Isaya 30:18).
Mungu ni mwenye rehema, neema na uvumilivu mwingi (Zaburi 86:15; Kutoka 34:6; Nehemia 9:17).
Uvumilivu ni sifa muhimu katika upendo wa kweli. Mtu hawezi kudai anakupenda ikiwa hana uvumilivu kwako.
Kumbuka kwamba kupenda kuna gharama. Mara nyingi mtu anayekuumiza zaidi ni yule unayempenda sana lakini pale ambapo kuna upendo wa kweli, uvumilivu huonekana. Kwa sababu ya changamoto za maisha, anayependa kwa dhati huendelea kusimama na kuvumilia.
2. Upendo hufadhili
Kufadhili ni kusaidia bila kutegemea au kusubiri malipo. Msaada huo unaweza kuwa wa kiroho, kifedha, mali au hata mawazo na ushauri.
Mtu anayetoa msaada wa namna hiyo huitwa mfadhili.
Kufadhili ni sifa muhimu ya upendo wa kweli kwa sababu huonyesha kuwa mtu yuko tayari kutumia rasilimali zake kwa ajili ya kuwasaidia wengine.
Mifano ya Kibiblia
Yesu aliwalisha wanaume elfu tano bila kuhesabu wanawake na watoto (Mathayo 14:14-21).
Yesu alimsaidia Petro na mitume kupata fedha za kulipa ushuru (Mathayo 17:24-27).
Eliya alimsaidia mjane kwa chakula kwa muda wa miaka mitatu na nusu (1 Wafalme 17:14-16).
Biblia imejaa mifano ya wafadhili kwa sababu Mfadhili wa kwanza ni Mungu mwenyewe.
Anayekupenda kwa kweli atakuwa tayari kuwa msaada kwako hasa pale unapokuwa na hitaji. Msaada wa kweli hautafutii faida wala masharti ya kulipwa. Upendo wa kweli hujitoa kwa moyo wa huduma na kujali.
3. Upendo hauhusudu
Kuhusudu ni kuwa na wivu mbaya au maumivu moyoni kwa sababu ya mafanikio, baraka, uwezo, mali, nafasi au maendeleo ya mtu mwingine.
Biblia inasema upendo hauhusudu. Hii ina maana kwamba mwenye upendo wa kweli hafurahishwi na kushindwa kwa wengine wala haumizwi na mafanikio yao.
Mtu anayesema anakupenda lakini anaumia kwa maendeleo yako bado hajajifunza upendo wa kweli.
Mifano ya Kibiblia
Ndugu zake Yusufu walimhusudu na hawakusema naye vizuri (Mwanzo 37:11). Sauli alimhusudu Daudi kwa sababu Daudi alipata kibali kikubwa zaidi (1 Samweli 18:9).
Kuhusudu ni tabia inayoweza kuzaa chuki, ugomvi na hata maangamizi. Kaini alimhusudu ndugu yake Abeli na baadaye akamuua lakini pale ambapo kuna upendo wa kweli, watu hufurahia mafanikio ya wenzao na kumshukuru Mungu kwa yale anayowatendea wengine.
Wapendwa, baada ya kujifunza somo hili, Mungu anatukumbusha kwamba upendo wa kweli siyo maneno matamu pekee bali ni maisha yanayoonekana katika matendo.
Upendo wa kweli huvumilia. Upendo wa kweli hufadhili. Upendo wa kweli hauhusudu.
Tunapoendelea na safari yetu ya wokovu, tuombe neema ya Mungu ili sifa hizi ziwe sehemu ya maisha yetu. Dunia inahitaji kuona upendo wa Kristo kupitia sisi. Familia zetu zinahitaji kuona upendo huo. Kanisa linahitaji kuona upendo huo. Hata wale wasiomjua Kristo wanahitaji kuuona upendo huo kupitia matendo yetu.
Ikiwa umekuwa ukikata tamaa kwa sababu ya changamoto za maisha, kumbuka kwamba Mungu bado anakupenda na anakuvumilia. Ikiwa umekuwa ukihitaji msaada, amini kwamba Mungu ndiye Mfadhili mkuu ambaye hataacha kukutunza. Na ikiwa umekuwa ukipambana na hisia za wivu au husuda, mwombe Roho Mtakatifu akupe moyo wa kufurahia mafanikio ya wengine.
Bwana akujaze upendo wake ndani yako ili uwe baraka kwa wengi na ushuhuda wa wema wake mahali popote utakapokuwa.
Mungu awabariki sana. Amina.
Kwa ushauri na maombezi Mchungaji Gasper Madumla anapatikana kwa simu: +255 781 001 002.