Dar es Salaam.  Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kupokea gawio na michango mingine kutoka mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa katika hafla ya Siku ya Gawio 2026 itakayofanyika Juni 30, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo inakuja wakati Serikali ikiongeza msisitizo katika kuhakikisha uwekezaji wa umma unaleta matokeo yanayopimika na kuongeza mchango wake katika mapato ya Taifa.

Gawio hili linatolewa pia wakati ambao Serikali imewekeza zaidi ya Sh92 trilioni katika mashirika na taasisi za umma ambazo zimekuwa zikiendelea kuzalisha faida.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Juni 15, 2026 Naibu Msajili wa Hazina, Lightness Mauki amesema mbali na kukabidhi fedha, siku ya gawio imekuwa jukwaa muhimu la kupima mafanikio ya uwekezaji wa Serikali na mchango wa mashirika ya umma katika ukuaji wa uchumi.

Hiyo ni kwa sababu katika hafla hiyo, taasisi za umma na kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa zitawasilisha gawio na michango mingine ya kisheria inayochangia mapato ya Serikali.

Mapato hayo hutumika kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, maji, nishati na miundombinu.

“Hii ni fursa ya kuonesha matokeo ya uwekezaji wa Serikali na namna taasisi za umma zinavyochangia maendeleo ya Taifa kupitia gawio na michango mingine inayowasilishwa serikalini,” amesema.

Amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni, “Uwekezaji wa Umma Wenye Matokeo: Nguzo ya Uchumi Shindani na Maendeleo Endelevu Kuelekea Dira 2050,” ambayo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha rasilimali zote zinazowekezwa kwa niaba ya wananchi zinazalisha matokeo yanayoonekana na kugusa maisha ya Watanzania.

Huu ni mwendelezo wa mashirika haya kutoa gawio kwa serikali jambo ambalo limekuwa likifanyika kila mwaka, kwa upande wa mwaka jana serikali ilipokea Sh1.028 trilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 68 kutoka Sh767 bilioni zilizopatikana mwaka juzi.

Lightness amesema uwepo wa siku hii pia unalenga kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa mali za umma kwa kuwapa wananchi nafasi ya kuona namna uwekezaji unaofanywa kwa niaba yao unavyozalisha thamani na mapato.

“Hadi Juni 2025, Serikali ilikuwa imewekeza zaidi ya Sh92 trilioni katika mashirika ya umma na kampuni mbalimbali, jambo linalofanya suala la ufanisi wa uwekezaji huo kuwa muhimu kwa maendeleo ya nchi. Wananchi ndio wamiliki wa rasilimali hizi hivyo wanapaswa kuona matokeo ya uwekezaji huo na namna unavyochangia katika maendeleo ya Taifa,” amesema.

Mbali na kupokea gawio, Rais Samia pia atatunuku tuzo kwa taasisi na kampuni zilizoonyesha utendaji bora na kutoa gawio kubwa zaidi kwa Serikali katika mwaka wa fedha uliopita.

Hatua hiyo inalenga kuhamasisha ushindani wa kibiashara, uwajibikaji na usimamizi unaozingatia matokeo katika mashirika ya umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *