Mji mkuu wa Port-au-Prince umekuwa ukikumbwa na vurugu za magenge kwa miaka kadhaa, huku makundi zaidi ya 20 yenye silaha yakidhibiti sehemu kubwa ya jiji na maeneo ya jirani. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, zaidi ya watu 2,300 wameuawa na wengine zaidi ya 1,100 kujeruhiwa kutokana na ghasia hizo.

© BINUH Vikosi vya kukandamiza Magenge ya uhalifu viko katik akambi ya Vertières mashariki mwa mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince.

Kikosi cha GSF kimeanza kufanya doria katika maeneo mbalimbali ya Port-au-Prince kwa lengo la kurejesha usalama, kulinda raia na kuwezesha misaada ya kibinadamu kuwafikia wanaohitaji. Umoja wa Mataifa kupitia Ofisi yake ya Msaada nchini Haiti (UNSOH) unatoa msaada wa kiufundi, vifaa, huduma za afya na usafiri ili kusaidia kikosi hicho kutekeleza majukumu yake.

Akiwa ziarani nchini Haiti, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alitembelea kambi ya kikosi hicho na kueleza matumaini yake kuhusu hatua hiyo mpya. “Kupelekwa kwa kikosi hiki kunatoa fursa halisi ya kupunguza vurugu na kurejesha mamlaka ya dola. Hatuna haki ya kupoteza fursa hii,” alisema.

© WFP Haiti

Katibu Mkuu Guterres amesisitiza kuwa suluhisho la kudumu haliwezi kupatikana kwa nguvu za kijeshi pekee. Alisema magenge yanapaswa kuvuliwa silaha, kuvunjwa na wanachama wake kurejeshwa katika jamii kupitia mchakato unaoongozwa na Wahaiti wenyewe. “Usalama pekee hautoshi; lazima uambatane na maendeleo ya kisiasa.”

Nchi ya Haiti imeshuhudia miaka kadhaa ya ukosefu wa utulivu hali ambayo imewalazimu takribani watu milioni 1.5 kuyahama makazi yao, huku mamilioni zaidi wakihitaji msaada wa kibinadamu kutokana na kuongezeka kwa umaskini. Haiti pia imeendelea kukabiliwa na ombwe la kisiasa tangu kuuawa kwa Rais wa zamani Jovenel Moïse mwaka 2021. 

Wakati wa ziara yake, Guterres alikutana na familia zilizolazimika kukimbia makazi yao kutokana na vurugu za magenge. 

“Nimekutana na familia ambazo zimepoteza kila kitu lakini bado zinaendelea kusimama pamoja kwa ujasiri na heshima inayostahili kupongezwa,” alisema Guterres. “Familia hizi haziitaji huruma yangu; zinasubiri hatua kuchukuliwa.”

© WFP Wanawake wawili wameketi kando ya ukuta wa zege, wakisuka nywele nchini Haiti.

Licha ya changamoto zinazoendelea, matumaini mapya yanaonekana kujitokeza. Doria za miguu, vituo vya operesheni katika maeneo mbalimbali na juhudi za kuzuia usafirishaji haramu wa silaha zinatarajiwa kudhoofisha uwezo wa magenge kuendelea kufanya mashambulizi.

Akihitimisha ziara yake, Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema, “Kwa mara ya kwanza katika miaka mingi, kuna mwanga mwishoni mwa handaki. Haiti ina nafasi ya kuanza ukurasa mpya, lakini hilo litawezekana tu ikiwa jumuiya ya kimataifa itatimiza wajibu wake.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *