Monica Juma, ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), anavunja rekodi kwa kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika Mashariki na Kusini mwa dunia kushika nafasi hiyo ya juu katika taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Picha ya UN/Eskinder Debebe Hafla ya Kuapishwa kwa Katibu Mkuu, Bi. Monica Juma, Mkurugenzi Mtendaji, Ofisi UMOJA WA MATAIFA ya Dawa za Kulevya na Uhalifu na Mkurugenzi Mkuu, Ofisi UMOJA WA MATAIFA huko Vienna.

Kwa Bi. Juma, uteuzi huo si mafanikio yake binafsi pekee, bali ni ishara ya kutambuliwa kwa mchango wa Waafrika katika uongozi wa kimataifa.

“Hili ni jambo zuri sana. Limetupa heshima kubwa. Linadhihirisha kwamba kuna watu ambao ni watendakazi katika Afrika,” anasema kwa furaha huku akieleza kuwa anathamini nafasi hiyo ya kuitumikia dunia nzima.

Kwanza kusikiliza kabla ya kuongoza

Tofauti na viongozi wengi wanaoingia ofisini na mipango mikubwa tayari mikononi mwao, Bi. Juma anaanza safari yake kwa kusikiliza.

Anasema muda wake wa mwanzo akiwa Vienna, Austria, makao makuu ya UNODC, anautumia kuwasikiliza wafanyakazi, viongozi wa Umoja wa Mataifa na timu zake zilizoko katika ofisi za kikanda na nchi mbalimbali duniani.

Lengo lake ni kuelewa kwa kina namna taasisi hiyo inavyofanya kazi kabla ya kuamua hatua zinazofuata.

“Kwanza nataka kuelewa kazi zinafanyika vipi ili tuzipeleke mbele,” anasema.

Uhalifu wa kisasa ni mtandao mmoja mkubwa

Kwa mujibu wa Bi. Juma, changamoto kubwa ya sasa ni kwamba aina mbalimbali za uhalifu hazifanyiki tena kwa kujitegemea.

Anasema biashara ya dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa binadamu, utakatishaji fedha na makundi ya kihalifu ya kimataifa sasa yameunganishwa katika kile kinachoitwa mtandao wa Kimataifa wa Uhalifu.

“Huwezi kuangalia tatizo moja ukaacha mengine. Yote yanashikamana kama mtandao,” anafafanua.

Kutokana na hali hiyo, anaamini ushirikiano wa kimataifa ndiyo silaha muhimu zaidi katika kukabiliana na uhalifu wa kisasa.

Akisisitiza kuwa “Mataifa yanahitaji kushirikiana, kubadilishana taarifa na kusaidiana katika uchunguzi na utekelezaji wa sheria.”

UN News Monica Juma, ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) akizungumza na Flora Nducha wa UN News Kiswahili.

Wanawake na watoto katika mstari wa mbele wa hatari

Jambo linalomsumbua zaidi Bi. Juma anasema ni kuongezeka kwa hatari zinazowakabili wanawake na watoto, hasa kupitia teknolojia na mitandao ya kijamii.

Anasema vijana wengi wanadanganywa na kuingizwa katika mitandao ya kihalifu bila familia zao kutambua.

“Anaweza kuwa nyumbani, unafikiri mtoto yuko chumbani kwake, kumbe tayari ameshikiliwa na mtandao wa kihalifu kupitia mtandaoni,” anaonya.

Kwa mtazamo wake, suluhisho linahitaji zaidi ya sheria kali pekee. Linahitaji mifumo madhubuti ya kushirikiana kati ya vyombo vya sheria, mashirika ya kimataifa na jamii ili kuwabaini wahalifu mapema na kuwalinda walio hatarini.

Afrika Mashariki: Kutoka njia ya kupitisha dawa hadi soko lenyewe

Akiangazia eneo analolifahamu vizuri la Afrika Mashariki, Monica Juma anasema mabadiliko makubwa yamejitokeza katika biashara ya dawa za kulevya.

Kwa miaka mingi, nchi za eneo hilo zilikuwa zikitumika kama njia ya kusafirisha dawa kwenda Ulaya na maeneo mengine. Hata hivyo, hali imebadilika.

“Kwa sasa Kenya, Tanzania na Uganda zimekuwa maeneo ya matumizi pia. Watoto wetu wako hatarini,” anasema.

Anasisitiza umuhimu wa kuanza mapambano hayo mapema kabisa kupitia elimu mashuleni. Watoto wanapaswa kufundishwa kutambua ishara za hatari, kujua namna ya kujilinda na kuripoti vitendo vinavyotia shaka. anasema

Lakini kwa wale ambao tayari wameathirika na uraibu wa dawa za kulevya, anasema jamii zinahitaji kuwekeza katika huduma za ushauri nasaha na vituo vya kurekebisha tabia badala ya kutegemea adhabu pekee.

“Tunapowapeleka watoto magerezani bila kuwasaidia, tunaharibu maisha yao zaidi,” anasema.

Picha ya UN/Manuel Elías Bi. Monica Juma, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya UMOJA WA MATAIFA huko Vienna na Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya UMOJA WA MATAIFA ya Dawa za Kulevya na Uhalifu, akizungumza katika Ukumbi wa Mkutano Mkuu.

Kuwapa nafasi ya pili maishani badala ya hukumu pekee

Katika maono yake, mapambano dhidi ya dawa za kulevya na uhalifu yanapaswa kuanzia katika kinga, elimu na fursa za maisha.

Anasisitiza kuwa vijana wanahitaji ajira, stadi za maisha na matumaini ya kesho. Bila hivyo, wanaweza kuvutwa kwa urahisi katika makundi ya kihalifu.

Anasema “Lazima tuwape kazi na fursa ili wasiwe majangili au washiriki wa magenge,”

Nguvu ya matumaini

Licha ya ukubwa wa changamoto zinazolikabili dunia, Monica Juma bado ana matumaini makubwa.

Chanzo cha matumaini hayo ni imani yake kwamba kila binadamu anatamani maisha yenye heshima na usalama.

“Hakuna mtu ambaye hatamani maisha ya heshima,” anasema.

Kwa mtazamo wake, kila mtu ana jukumu la kutekeleza kuanzia wazazi, walimu, viongozi wa jamii, serikali hadi mashirika ya kimataifa.

Anahitimisha kwa ujumbe rahisi lakini wenye nguvu, dunia salama bila uhalifu haiwezi kujengwa na taasisi pekee; inahitaji mchango wa kila mmoja wetu. Kila mtu ana kazi ya kufanya.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *