Marekani. Kwa wengi, jina la Kate Ferdinand lilijulikana kupitia kipindi cha televisheni cha The Only Way Is Essex (TOWIE). Hata hivyo, safari yake ya maisha ilibadilika kabisa alipokutana na aliyekuwa nahodha wa timu ya taifa ya England na nyota wa Manchester United, Rio Ferdinand.
Kate alizaliwa Juni 3, 1991 huko Essex, England. Kabla ya kuingia kwenye ulimwengu wa televisheni na umaarufu. Alikuwa akifanya kazi kama meneja wa msaada wa biashara katika sekta ya benki.
Umaarufu wake ulianza kuongezeka alipohusishwa kimapenzi na Dan Edgar, mmoja wa washiriki wa kipindi cha TOWIE, kabla ya yeye mwenyewe kujiunga na kipindi hicho mwaka 2015.
Ingawa maisha yake yalionekana kwenda vizuri katika ulimwengu wa burudani. Kate hakutarajia kwamba angejikuta katika jukumu kubwa la kuwa mama wa kambo wa watoto watatu waliokuwa wamepitia maumivu makubwa ya kumpoteza mama yao.
Kukutana na Rio Ferdinand
Kate na Rio walikutana kupitia marafiki walipokuwa likizoni Dubai mwaka 2017. Wakati huo, Rio alikuwa bado akijaribu kujenga upya maisha yake baada ya kumpoteza mke wake wa kwanza, Rebecca Ellison, aliyefariki kutokana na saratani ya matiti mwaka 2015 akiwa na umri wa miaka 34.
Kabla ya hapo, Rebecca na Rio walikuwa wamejenga familia yenye watoto watatu: Lorenz, Tate na Tia. Kifo cha Rebecca kilimuacha Rio akiwa mzazi mmoja na mwenye jukumu la kuwalea watoto hao huku akipambana na huzuni ya kumpoteza mke wake.
Mwaka 2017, Rio alitoa makala maalumu kupitia BBC iliyozungumzia maisha yake kama baba anayelea watoto peke yake baada ya msiba huo. Makala hiyo ilitazamwa na zaidi ya watu milioni saba na kuwagusa watu wengi.
Rio anakumbuka kipindi hicho kama moja ya nyakati ngumu zaidi maishani mwake.
“Nilikuwa nimevunjika moyo kabisa. Nilihisi kama nisingeweza kutoka katika hali ile ngumu. Kisha nikakutana na Kate, na kila kitu kikabadilika.”
Changamoto za Kuwa Mama wa Kambo
Wakati Kate alipoanza uhusiano wake na Rio, alikuwa na umri wa miaka 27 tu. Anakiri kwamba hakujua kikamilifu changamoto zilizokuwa mbele yake.
“Mama yangu alidhani nimechanganyikiwa,” aliwahi kusema akielezea jinsi familia yake ilivyoshangazwa na uamuzi wake wa kuingia kwenye uhusiano na mwanaume aliyekuwa mkubwa kwake kwa miaka 12, mwenye watoto watatu na aliyekuwa amepitia huzuni kubwa ya kumpoteza mke wake.
Kate alikiri kuwa awali alidhani jukumu hilo lingekuwa rahisi kuliko lilivyokuwa kwa uhalisia.
“Nilipoingia katika familia hii nilifikiri mambo yangekuwa rahisi, lakini ukweli ni kwamba yanahitaji kazi kubwa sana.”
Kabla ya hapo, maisha yake yalikuwa tofauti kabisa. Alikuwa amezoea kujijali mwenyewe, kula migahawani na kutumia muda wake kwa shughuli za burudani. Ghafla alijikuta akiwajibika kwa watoto watatu waliokuwa wakihitaji upendo, utulivu na msaada wa kihisia.
Anasema mabadiliko hayo yalikuwa makubwa sana kwake.
“Nilikuwa nimezoea kujijali mwenyewe tu. Ghafla nikawa nawalea watoto watatu na kuweka mahitaji yao mbele ya yangu.”
Kukabiliana na hukumu za umma
Kutokana na umaarufu wa Rio na historia ya Kate katika televisheni ya uhalisia, uhusiano wao ulivutia mijadala mikubwa mitandaoni.
Watu wengi walihisi Rio alikuwa ameanza uhusiano mpya haraka sana baada ya kifo cha Rebecca. Maoni hayo yalimuumiza Rio.
“Unapoona watu wakisema, ‘Amesonga mbele haraka sana,’ unafikiria, sawa, lakini natumai hamtapitia hali kama hii maishani mwenu.”
Kwa upande wake, Kate alikuwa na mtazamo tofauti. Alisema alielewa kwa nini baadhi ya watu walikuwa na mashaka.
“Watu walikuwa na haki ya kunihukumu. Unapoona mtu mpya anaingia kwenye familia kama hii, ni kawaida kujiuliza kama atakuwa mfano mzuri kwa watoto.”
Hata hivyo, badala ya kujibu ukosoaji huo kwa maneno, Kate aliamua kuthibitisha uwezo wake kupitia vitendo na kujenga mahusiano ya karibu na watoto wa Rio.
Harusi na familia mpya
Baada ya miaka miwili ya uhusiano, Kate na Rio walifunga ndoa nchini Turkey tarehe 27 Septemba 2019.
Watoto wa Rio walikuwa sehemu muhimu ya sherehe hiyo. Binti yake Tia hata alipewa jukumu maalumu katika harusi hiyo, jambo lililoonyesha ukaribu uliokuwa umejengwa kati yao.
Mwaka 2020, wanandoa hao walitangaza kuwa walikuwa wanatarajia mtoto wao wa kwanza pamoja. Mtoto wao wa kiume alizaliwa tarehe 18 Desemba 2020, na kuongeza furaha mpya ndani ya familia hiyo.
Baadaye familia yao iliendelea kukua huku Kate akizidi kuzoea jukumu lake kama mama wa kambo na mama wa watoto wake mwenyewe.
Kuacha umaarufu kwa ajili ya familia
Tofauti na maisha yake ya awali kwenye TOWIE, Kate aliamua kupunguza sana shughuli zake kwenye televisheni na kujikita zaidi katika familia.
Anasema alitambua kwamba watoto wa Rio walihitaji mtu wa kuwa karibu nao nyumbani kuliko mtu anayekuwa mbali muda mwingi.
“Nilijua kwamba watoto hawa waliompoteza mama yao walihitaji mtu wa kuwa karibu nao nyumbani, si mtu anayekuwa nje muda wote.”
Kwa miaka iliyofuata, Kate alijikita zaidi katika shughuli za mitandao ya kijamii, biashara zake binafsi na malezi ya watoto.
Mwaka 2025, yeye na Rio walifanya uamuzi mkubwa wa kuhamia katika United Arab Emirates, wakieleza kuwa walivutiwa na ubora wa elimu na maisha bora kwa watoto wao.
Mwanamke aliyeleta mwanzo mpya
Kwa Rio Ferdinand, Kate amekuwa zaidi ya mke. Amekuwa mshirika aliyesaidia familia yake kujijenga upya baada ya kipindi kigumu cha huzuni na majonzi.
Safari yao imeonyesha kwamba familia za wazazi wa kambo zinaweza kufanikiwa licha ya changamoto zinazoweza kujitokeza. Ingawa Kate aliingia katika maisha ambayo hakuyatarajia akiwa na umri wa miaka 27, ameweza kujenga uhusiano wa karibu na watoto wa Rio na kuwa sehemu muhimu ya familia hiyo.
Kutoka kuwa nyota wa televisheni ya uhalisia hadi kuwa mama wa kambo anayeheshimika na mshawishi wa mitandao ya kijamii, Kate Ferdinand ameonyesha kwamba wakati mwingine mapenzi huweza kuleta majukumu makubwa, lakini pia huweza kuleta nafasi ya kuandika upya simulizi la maisha ya mtu.