
Ripoti hiyo inaonesha taswira ya kutisha ya utoto unaozidi kutawaliwa na mawimbi ya joto kali, ukame wa muda mrefu, mafuriko makubwa na dhoruba zinazozidi kuwa za mara kwa mara duniani.
“Maisha ya watoto yanaendelea kuvurugwa na athari za mawimbi ya joto, moto wa nyika, ukame na mafuriko,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell.
“Kwa sasa, nusu ya watoto duniani wanaishi huku wakikabiliwa na angalau vitisho vitatu vya tabianchi vinavyoathiri maisha yao ya kila siku.” Ameongeza.
Ripoti hiyo, iliyopewa Kichwa “Ripoti ya hatari za tabianchi kwa watoto 2026”, imechambua maeneo ambayo watoto wanaishi na kufichua namna wanavyokumbwa na majanga manane makuu ya tabianchi pamoja na changamoto nyingine zinazoongeza hatari kama vile ukosefu wa huduma za afya, maji safi na elimu.
Majanga yanayokuja kwa pamoja
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, karibu kila mtoto duniani anakabiliwa na angalau tishio moja la tabianchi, huku zaidi ya watoto milioni nne wakikabiliwa na majanga sita tofauti kwa wakati mmoja.
Ukame, joto kali na mawimbi ya joto vimetajwa kuwa mchanganyiko unaoathiri watoto wengi zaidi duniani, ambapo zaidi ya watoto milioni 296 wanaishi katika maeneo yanayokumbwa na hali zote tatu kwa pamoja.
Mchanganyiko wa pili kwa ukubwa ni ukame, joto kali na dhoruba za kitropiki, vinavyowaathiri zaidi ya watoto milioni 115 duniani.
UNICEF imesema kwa mara ya kwanza ripoti hii inaonesha si tu maeneo yanayokumbwa na majanga hayo, bali pia ukubwa wake na jinsi yanavyoingiliana, hali inayowafanya watoto kuwa katika hatari kubwa zaidi.
Sahel yaongoza kwa maumivu Afrika
Ukanda wa Sahel barani Afrika umetajwa kuwa miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi.
Zaidi ya watoto milioni nne katika eneo hilo wanakabiliwa kwa wakati mmoja na mawimbi ya joto, joto kali na dhoruba za mchanga na vumbi.
Aidha, nchi za Asia ikiwemo Bangladesh, Myanmar na Pakistan zimeonekana kuwa na viwango vya juu zaidi vya watoto wanaokabiliwa na majanga mengi ya tabianchi kwa wakati mmoja na kwa ukali mkubwa zaidi kuliko sehemu nyingine duniani.
Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa watoto wanaoishi katika nchi dhaifu na zisizo na bandari kama Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, wanabeba mzigo mara mbili, wanakumbwa na majanga ya tabianchi huku wakikosa huduma muhimu za msingi zinazoweza kuwasaidia kuhimili na kujikwamua baada ya majanga hayo.
Hata mataifa tajiri hayajasalimika
UNICEF imeonya kuwa mgogoro wa tabianchi hauchagui nchi maskini pekee.
Nchini Italia, kwa mfano, zaidi ya watoto milioni sita wanakabiliwa na ukame na mawimbi ya joto ya muda mrefu.
Hata hivyo, shirika hilo linasema Italia ni mfano wa namna uwekezaji katika hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unavyoweza kupunguza hatari zinazowakabili watoto.
Uchafuzi wa hewa na malaria vyaongeza hatari
Mbali na majanga ya hali ya hewa, ripoti hiyo imechunguza pia athari za uchafuzi wa hewa na malaria, ambazo zote zina uhusiano mkubwa na mabadiliko ya tabianchi.
Takwimu zinaonesha kuwa karibu kila mtoto duniani anaathiriwa na uchafuzi wa hewa, huku watoto bilioni moja wakiishi katika maeneo yenye hatari ya malaria.
Kwa watoto ambao tayari wanakabiliwa na majanga mengi ya tabianchi, changamoto hizi zinaongeza mzigo mwingine wa kiafya na kijamii.
UNICEF yataka hatua za dharura
Kutokana na hali hiyo, UNICEF imezitaka serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kuchukua hatua za haraka kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa watoto.
Shirika hilo limetoa wito wa kupunguzwa kwa uzalishaji wa gesi chafuzi, kuondolewa kwa utegemezi wa mafuta ya kisukuku na kuharakisha matumizi ya nishati mbadala.
Pia limetaka uwekezaji mkubwa katika shule zinazostahimili majanga, vituo vya afya vinavyokabiliana na athari za tabianchi, mifumo ya maji safi na mifumo ya tahadhari za mapema inayowalinda watoto.
Kulinda watoto leo ni kuilinda kesho yetu
Russell amesema ripoti hiyo inaweza kusaidia serikali kupanga kwa usahihi zaidi na kuelekeza rasilimali katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.
“Uchambuzi huu unaweza kusaidia serikali na watunga sera kupanga vizuri zaidi na kuwekeza kwa ufanisi katika huduma zenye mnepo dhidi ya majanga,” amesema.
“Tunapoimarisha mifumo ya afya na elimu, na kuboresha miundombinu kwa kuzingatia mahitaji ya watoto, tunawalinda dhidi ya vitisho vya leo na kuhakikisha mustakabali wao wa kesho.”
Kadri majanga ya tabianchi yanavyozidi kuongezeka na kuingiliana, ujumbe wa UNICEF ni wazi, kulinda watoto dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi si suala la kesho tena, bali ni jukumu la dharura linalohitaji hatua leo.