
Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran, Gholamhossein Mohseni Ejei, amesema Iran iko tayari kuendeleza mapambano dhidi ya uchokozi wa Marekani na Israel iwapo maadui hawatatimiza ahadi zao chini ya makubaliano mapya yaliyotangazwa ya kumaliza vita.
Akizungumza mbele ya mkutano wa majaji na watumishi wa Mahakama ya Juu ya Iran siku ya Jumanne jijini Tehran, Mohseni Ejei amesema kwamba licha ya Iran kukubali waraka wa makubaliano (MoU) na Marekani unaolenga kukomesha vita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuwa macho na itachukua hatua madhubuti endapo maadui watakiuka makubaliano hayo.
Amesema: “Adui huyu mwenye hila, mhalifu na mwenye nia ovu hawezi kuaminika kwa hali yoyote; ni lazima tuwe macho, na tayari tuko macho. Adui anafahamu vyema anakabiliana na nani.”
Ameongeza kuwa Iran iko tayari kurejea katika mapambano iwapo upande wa adui utavunja ahadi zake wakati wa mchakato wa mazungumzo ya siku 60 yatakayoanza baada ya kutiwa saini kwa waraka huo wa makubaliano siku ya Ijumaa. Mazungumzo hayo yanatarajiwa kujumuisha masuala yanayohusu mpango wa nyuklia wa Iran pamoja na kuondolewa kwa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya nchi hii.
Afisa huyo wa juu wa mahakama, ambaye pia anaongoza moja ya mihimili mitatu ya dola ya Iran, amesema wawakilishi wa Iran katika mazungumzo na Marekani hawatatoa mwanya wa kukiukwa kwa haki za taifa la Iran wakati wa majadiliano hayo.
Aidha amesema wajumbe wa mazungumzo watajitahidi kulinda haki za makundi ya muqawama yaliyo na uhusiano na Iran katika nchi nyingine, zikiwemo Lebanon, Palestina na Yemen.